Namungo kuwavaa ihefu bila Duah

Thursday April 08 2021
NAMUNGO PC
By Ramadhan Elias

LEO Alhamisi katika uwanja wa Majaliwa Stadium uliopo Lindi kutapigwa na mechi ya Ligi Kuu Bara ambapo wenyeji Namungo watakuwa wakiikaribisha Ihefu kutoka Mbeya.


Katika mchezo huo unaotarajia kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila timu kutaka kusogea juu kutoka nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi Namungo wakiwa nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi 18 na kuvuna alama 27 huku Ihefu wakiwa nafasi ya pili kutoka mwisho (17) baada ya kucheza mechi 24 na kuambulia alama 20 pekee, Namungo watamkosa beki wao tegemeo Stephen Dua aliyepata majeraha. 
Akizungumza na Mwanaspoti kocha mkuu wa Namungo Hemed Seleman 'Morocco' amethibitisha kuumia kwa beki huyo na kuelezea namna walivyojipanga kuelekea mechi hiyo.


“Tunatambua ubora wa Ihefu na kuwa ipo chini kwenye msimamo wa ligi lakini si timu mbaya  ya kubeza, ukiangalia wachezaji wake wengi wana uzoefu na wanaweza kupata matokeo katika mechi yeyote.

Sisi tupo tayari kupambana nao na kutafuta ushindi, wachezaji wetu wote wapo fiti kasoro beki Stephen Duah aliyepata majeraha ya mguu ndiye tutamkosa kwenye mechi ya leo," Amesema Morocco.


Duah anayecheza eneo la beki wa kati amekuwa mhimili mkubwa kwenye kikosi cha Namungo katika mashindano yote timu hiyo inayoshiriki yakiwemo yale ya kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo kwa nyakati tofauti amekuwa akipangwa na Carlos Protos ama Frank Magingi.


Mchezo wa Mapema leo utazikutanisha Mbeya City na Namungo saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Sokonne Mbeya. 

Advertisement
Advertisement