Namungo bado mambo magumu Angola

NI kama sinema vile kwa kile kinachoendelea kuikumba timu ya Namungo nchini Angola wakiwasubiri wachezaji wao watatu na Mtendaji Mkuu wao ambao waliwekwa karantini kwa madai ya kuwa na virusi vya corona.
Namungo wamekumbana na kadhia hiyo siku ya tatu sasa, toka walipofika Nchini humo na kuzuiliwa kwa madai ya Lucas Kikoti, Fred Tangalu na Khamis Faki kudaiwa kuwa na virusi hivyo sambamba na Mtendaji Mkuu Omary Kaaya.
Mkuu wa Idara ya habari ya klabu hiyo Kindamba Namlia ameiambia Mwanaspoti kuwa, wao hawawezi kuondoka Nchini humo kama watu hao wanne hawajaachiwa.
"Ni ngumu kuondoka japokuwa tuna ndege yetu ya kukodi, kwani wachezaji wetu watatu na kiongozi wetu wameshikiliwa kwa madai ya kuwa na maambukizi ya virusi vya corona hivyo hatuwezi kuondoka tukawaacha," amesema Namlia
Namlia amedai walichokifanya wapinzani wao Primeiro De Agosto ni jambo baya na la mipango kwa madai sio jambo la kawaida ambalo wamefanyiwa mpaka hivi sasa.
"Hili suala ni kama figisu za mpira lakini sio hii ni uhalifu, umepangwa na mamlaka mbalimbali afya, anga, uhamiaji, ulinzi na usalama pamoja na Shirikisho lao, hiki kitu sio kabisa,"
"Walichokifanya kama ingekuwa ni sinema basi ingeonekana kwenye sinema za Sylvester Stallone 'Rambo' au Arnold Schwarzenegger kwa sinema zetu za bongo movi huwezi kuona matukio ya kikatili kama haya, hiki kitu walichokifanya kinatakiwa kupingwa na kila mtu,"anasema.
Namungo wameshindwa kucheza mchezo wao huo wa kombe la Shirikisho kutokana na sintofahamu hiyo iliyopelekea CAF kuipiga chini mchezo huo.