Nabi: Yanga hii itachukua sana Bara
Muktasari:
- Kocha huyo aliyeitumikia timu hiyo kwa misimu miwili anaendelea kufuatiliaYanga japokuwa sasa anaifundisha FAR Rabat ya Morocco ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu nchini humo.
KOCHA wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi ametoa tahadhari kwa timu zingine Ligi Kuu Bara kutokana na moto ilionao Yanga akisema kama hazitakaza, basi ubingwa zitausikia katika bomba kwa miaka mingi ijayo.
Nabi ambaye msimu uliopita aliumaliza kwa mafanikio akiwa na kikosi hicho kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA), Ngao ya Jamii na kutinga fainali ya ya Kombe la Shirikisho Afrika amesema Yanga ya sasa inaweza kubeba ubingwa wa Bara hata mara 10 mfululizo.
Kocha huyo aliyeitumikia timu hiyo kwa misimu miwili anaendelea kufuatilia kikosi hicho japokuwa sasa anaifundisha FAR Rabat ya Morocco ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu nchini humo.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa simu, Nabi amesema kitendo cha Yanga kuchukua ubingwa huo mara ya tatu mfululizo kinathibitisha ubora wa timu na utulivu wa uongozi wake.
Amesema Yanga kwa aina ya kikosi ilicho nacho ambacho sehemu kubwa alifanya nacho kazi anaamini kwamba bado kina nguvu ya kuendelea kutamba zaidi kwa kuchukua makombe.
"Yanga kuwa bingwa ni kitu ambacho hakijanishtua kwani timu na mwendo wao tangu walipoanza ligi walionyesha kuwa ni timu inayoishi kwa hesabu za kutaka ubingwa huo. Ukiziangalia timu shindani kwa Yanga kwenye mbio za ubingwa zilikuwa zinajitofautisha, angalia Simba timu yao ilikuwa na changamoto nyingi za ubora lakini kubwa ni kubadilisha makocha katikati ya msimu,” amesema.
"Azam walikuwa na timu nzuri ndio maana unaona imegawana pointi na Yanga. Shida yao ni kukosa mwendelezo kwenye mechi hapa ndipo walipoanguka. Kama hizi timu pinzani hazitajipanga sitashangaa kuona Yanga wanaweza kuchukua zaidi makombe haya kwa muda mrefu."
Nabi ameusifu uongozi wa Yanga kwa mafanikio hayo akisema ramani kubwa ya ushindi inaanzia hapo.
"Nimefanya kazi Yanga ukiacha mashabiki ambao siku zote wanatamani kuona timu inashinda, lakini presha kutoka kwa viongozi wao. Viongozi wa Yanga wana hesabu za mbali sana kwenye mechi, lakini pia unaona wana utulivu sana wakifanya mambo yao na hapa ndipo hesabu sahihi za kuijenga timu zinapotimia," amesema.
Baada ya ushindi katika mchezo wa juzi Jumatatu, Mei 13, mbele ya Mtibwa Sugar ilioshinda mabao 3-1, Yanga ilijihakikishia kombe la 30 la Ligi Kuu Bara.