Nabi: Mtaona mengi sana

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi ametamba kwamba mashabiki wataona mengi mazuri kwenye kikosi chake msimu huu.
Nabi ametamba kwamba kilichofanyika kwenye mechi mbili zilizopita ikiwemo waliyoshinda 2-1 dhidi ya Simba na kutwaa Ngao ya Jamii Jumamosi ni mwanzo tu kwani bado wanajaribu mambo mengi.
Alisema msimu uliopita kuna mechi alicheza timu yake ikiwa na shida katika baadhi ya maeneo kama beki wa kushoto, mawinga kushoto na kulia na hata katika nafasi ya kiungo.
Alisema kwenye mechi dhidi ya Simba mabadiliko ya Ducapel Moloko na Bernard Morrison yalikwenda kuongeza makali ya kikosi haswa wakati wa kushambulia na kuishika mechi tofauti na ilivyokuwa kipindi cha kwanza.
“Katika mechi hiyo kulingana na Simba ilivyokuwa imara kipindi cha kwanza nilibadilisha wachezaji nafasi ya kucheza Aziz Ki nilimtoa pembeni na kumtumia nyuma ya straika namba kumi alifanya vizuri zaidi ikiwemo kutoa pasi ya mwisho,” alisema Nabi na kuongeza;
“Moloko hakuwa sawa kisaikolojia baada ya kuwepo na taarifa nyingi (zikidai kuwa ataachwa ama atatolewa kwa mkopo), nilikaa naye chini kumtengeneza kiakili na mbinu, ameenda kufanya vizuri katika mechi ya Simba na naamini utakuwa muendelezo wake huo hadi katika mechi nyingine,”
“Morrison alifanya vizuri katika kushambulia kupitia pembeni iliwafanya hata mabeki wa wapinzani kushindwa kuja upande wetu na muda wote hawakuwa huru hili ndio nilikuwa nalitaka hata msimu uliopita hatukuwa nalo.
“Ushindi dhidi ya Simba umetupa morali na hali nzuri na kutamani kufanya vizuri zaidi na mechi hizo za mwanzo ni jambo jema kupata ushindi ili kuanza kukusanya pointi mapema kabla ya wakati wa presha kufika. Nitaendelea kutengeneza kikosi imara, bado tuna deni kubwa.”