Nabi ashtukia mtego wa Bara

YANGA ipo Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2022, lakini kocha wake aliyepo Ubelgiji kuna hesabu kali anazipiga ambazo ziliwafukuzisha watatu msimu uliopita kisa ubingwa.

Nabi akiwa kwake nchini Ubelgiji ameangalia ratiba ya ligi kisha kugundua itakaporejea tu Januari 16 itatakiwa kuifuata Coastal Union ya Tanga.

Alipoangalia matokeo ya mchezo kama huo msimu uliopita akagundua kwamba ndio ambao Yanga ilipoteza wa kwanza baada ya kucheza mingi bila kupoteza kama ambavyo wako sasa.

Yanga imekuwa ikipata wakati mgumu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga licha ya kuinyanyasa timu hiyo inapokuwa Dar es Salaam.

Msimu uliopita Yanga ilianza vyema na ilikuwa ikilinda rekodi ya kucheza mechi 32 za Ligi Kuu bila kupoteza, lakini ilipotua Mkwakwani ilipasuka 2-1, huku winga wa wana Jangwani wakati huo, Tuisila Kisinda alikosa penalti, japo aliwafungia bao la kufutia machozi.

Msimu huu, baada ya mechi hiyo ya Mkwakwani, Yanga itaifuata Polisi Tanzania Januari 23 Ushirika mkoani Kilimanjaro na katika mchezo kama huo msimu uliopita ilipata sare ambayo iliwafukuzisha kazi makocha watatu akiwemo msaidizi wake Cedric Kaze wakati huo akiwa kocha mkuu.

Mbali na Kaze, pia ilimtimua aliyekuwa msaidizi wake wa kwanza Nizar Khalfan na kocha wa makipa Mrundi Vladimir Niyonkuru.

Nabi baada ya kuona ratiba hiyo ameliambia Mwanaspoti kwamba anajua mazingira yote magumu katika mechi hizo na tayari ametoa mipango yake kwa mabosi.

Kocha huyo ambaye atatua nchini siku moja kabla ya mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi itakayopigwa Januari 13, alisema kitu cha kwanza ananachotaka kiheshimiwe ni kwa wachezaji ambao hawapo nchini kuwasili kwa wakati kama ambavyo ruhusa zimetolewa.

“Nimewaambia viongozi kila mchezaji ambaye yuko nje anatakiwa kuheshimu muda ambao tumempa. Sitahitaji kuona mchezaji anatoka nje ya muda ambao tumempa. Kuna programu ambayo itaendelea wakati huu bila kujali uwepo wangu,” alisema Nabi.

“Hizo ni mechi ngumu sana ambazo tunatakiwa kuwa nazo makini ili tusiharibu kasi yetu katika ligi. Tunaposhinda mechi hizo ni kama tumeshinda mechi za nusu fainali na fainali.

“Tutaangalia pia jinsi ya kwenda Tanga hatutakiwi kuwafanya wachezaji wakachoka. Nimeangalia umbali kuna vitu ambavyo nitazungumza na viongozi kuangalia tutakubaliana vipi.”


WADAU WAONGEA

Akizungumzia mechi hizo, Tigana Lukinja, kocha kitaaluma alisema Yanga imekuwa ikipambana kusaka matokeo Mkwakwani dhidi ya Coastal na anatarajia kuona mchezo mzuri na wa ushindani kutokana na timu zote kuwa na makocha wenye mbinu.

“Coastal Union msimu huu wameanza vizuri chini ya kocha Melis Medo wamekuwa na uwiano mzuri wa matokeo tofauti na misimu ya nyuma. Ukiangalia pia kwa upande wa Yanga baada ya kuyumba misimu minne mfululizo msimu huu wamekuja kivingine kwa kusajili kikosi cha ushindani,|” alisema.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Akida Makunda alisema kipindi hiki ligi imesimama huku timu nyingine zikiendelea kushiriki mashindano na nyingine kupisha michuano hiyo makocha wasawazishe makosa.

“Kama kila timu itatumia vyema dirisha hili na muda huu kuweka sawa vikosi vyao kutakuwa na mchezo mzuri siku hiyo, japo nakumbuka mara ya mwisho Yanga alifungwa 2-1. Asipokuwa makini anaweza kukutana tena na kipigo,” alisema.