Nabi apangua wanne Yanga

Wakati Yanga ikibakiza dakika chache kushuka Uwanjani wakiwakaribisha wageni wao Mbao kocha mkuu wa timu hiyo Nesreddine Nabi amefanya mabadiliko manne katika kikosi chake.
Katika kikosi hicho ambacho kinashuka kucheza mchezo wake wa pili wa hatua ya mtoano wa Kombe la Azam Shirikisho katika Uwanja wa CCM Kirumba Nabi amefanya badiliko moja katika safu yake ya ulinzi.
Nabi amemuanzisha beki Paul Godfrey 'Boxer' ambaye anaziba nafasi ya Mkongomani Djuma Shaban ambaye amekwenda kujiunga na timu yake ya Taifa.
Hata hivyo Djuma ambaye amefungiwa mechi tatu kwa kosa la kumpiga mchezaji wa Polisi Tanzania katika mchezo wa ligi asingeweza kuwa sehemu ya mchezo wa leo.
Mbali na Boxer Nabi ameendelea kuwapa nafasi kipa Abutwalib Mshery,beki wa kushoto akiwa Yassin Mustapha wakati mabeki wa kati wakiwa nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto na Dickson Job.
Katika safu ya kiungo Nabi amefanya mabadiliko matatu akimuanzisha kiungo mkabaji Zawadi Mauya ambaye anachukua nafasi ya Khalid Aucho anayetumikia adhabu ya kuwa na kadi tatu za njano.
Mbali na Mauya pia ingizo jipya lingine ni kiungo Salum Abubakar 'Sure boy' ambaye anachukua nafasi ya Yannic Bangala ambaye naye amekwenda kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo.
Nabi pia amemuanzisha kiungo Dickson Ambundo aliyeifungia bao la ushindi timu yake katika mchezo wa ligi wa Polisi akiingia kwa mabadiliko lakini leo akianza kuja kuchukua nafasi ya Said Ntibazonkiza ambaye ni majeruhi.
Safu ya ushambuliaji Nabi amewaanzisha Farid Mussa na mfungaji wao kinara wa mabao Fiston Mayele.
Kwenye benchi Nabi amewapa nafasi kipa Eric Johola,mabeki wakiwa David Bryson,Ibrahim Bacca,viungo wakiwa Mapinduzi Balama,Chrispin Ngushi,washambuliaji Chico Ushindi,Deuse Kaseke na Denis Nkake