Nabi aishtukia Marumo, asema wameficha mastaa wanne

YANGA imewasoma wapinzani wao kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Marumo Gallants ya Afrika Kusini wakati ikichapwa nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya nchini humo, Mamelodi Sundowns lakini kocha wa timu hiyo Nasreddine Nabi akatamka sentesi fupi 'Achaneni nao hao Marumo mtego huo'.

Marumo inazidi kudidimia ligi ya kwao na inahitaji kushinda mchezo ujao huku ikiwaombea dua mbaya wapinzani wao wanaopambana kujinasua kushuka daraja, lakini Nabi ameshtukia akili ya wapinzani wao akisema watakuja na timu tofauti Jumatano Mei 10.

Nabi alisema anafahamu Marumo haikuwatumia wachezaji wake wanne ambao wanawatumia katika kutengeneza mashambulizi yao hatari katika mechi za Shirikisho na hawatabweteka na kiwango cha timu hiyo kwenye ligi.

Kocha huyo alisema akili ya Marumo ni kutaka kuweka rekodi tofauti wakiitaka fainali na Yanga wala haitafuatilia matokeo ambayo wanayapata kwenye mechi za ligi nchini kwao.

"Tumewaangalia lakini achaneni na hao jamaa wanacheza na akili zetu, kuna watu wao hatari wanne katika kiungo na beki wa pembeni mmoja hawajawatumia hii mechi ya jana (juzi usiku) na hao ndio watu wao hatari sijajua sababu lakini tunawajua,"alisema Nabi.

"Tumechukua baadhi ya vitu lakini hatutapoteza malengo yetu kwa kuangalia hayo matokeo ya ligi ya kwao, Yanga inatakiwa kuizingatia Marumo ya Kombe la Shirikisho, hao ndio wenyewe.

Aidha Nabi amewachimba mkwara wachezaji wake akiwataka kuwa makini kuzingatia maandalizi yao kwani hawataki kujiweka katika wakati mgumu kuruhusu bao katika mchezo wa nyumbani.

Alisema wapinzani wao wamekuwa na akili kubwa wanapocheza ugenini kutengeneza mazingira ya kwenda kuimaliza mechi kwao mtego ambao Yanga lazima iukimbie kwa kucheza kwa umakini dhidi yao.

"Tunatakiwa kuwa makini na huu mchezo wa nyumbani, watu wanasema tunatakiwa kushinda mabao mengi, wako sahihi, kwangu mimi ni tofauti kidogo tunachotakiwa ni kuwa makini tusiruhusu bao hapa kwetu lakini ushindi wowote utatupa akili kubwa kule kwao.

"Tunakwenda kucheza na timu ambayo imekuwa ikitafuta njia nzuri ya kushinda kwao kuanzia ugenini, tumeona kosa ambalo Pyramids walilifanya kwao na matokeo yake wakaadhibiwa ugenini, tunacheza na timu isiyotabirika na wanaocheza kwa nidhamu kubwa.

"Nimewaambia wachezaji wangu kama kuna mchezo tunatakiwa kuonyesha ukomavu wa nidhamu ya mchezo ni huu wa nyumbani, lakini ushindi wowote utatusaidia uwe wa bao moja au zaidi kitu bora kwetu ni kuwanyima njia ya kuanzia kwao."