Nabi afuata dawa ya Mazembe

Muktasari:

  • Kocha huyo aliyeivusha Yanga hadi robo fainali ya michuano hiyo ikiwa ni mara ya kwanza katika ushiriki wa timu hiyo hatua ya makundi na huku ikiongoza msimamo wa Kundi D, itaifuata TP Mazembe katika mechi ya mwisho ya kundi hilo itakayopigwa Aprili 2 jijini Lubumbashi.

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi ametimka nchini kwenda Ulaya, huku akitoa salamu ambazo hazitakuwa njema jijini Lubumbashi, DR Congo, akisema hesabu zake sasa ni kumaliza na ushindi katika mechi ya mwisho ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha huyo aliyeivusha Yanga hadi robo fainali ya michuano hiyo ikiwa ni mara ya kwanza katika ushiriki wa timu hiyo hatua ya makundi na huku ikiongoza msimamo wa Kundi D, itaifuata TP Mazembe katika mechi ya mwisho ya kundi hilo itakayopigwa Aprili 2 jijini Lubumbashi.

Katika mechi ya kwanza baina yao iliyochezwa Dar es Salaam Februari 19, Yanga ilishinda mabao 3-1 na mchezo ujao utakuwa kama wa kisasi kwa Wakongo hao dhidi ya Wanajangwani, lakini tayari Kocha Nabi amesema anaifuata dawa Ubelgiji anakoenda kwa mapumziko kabla ya kuwashukia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema Yanga haijamaliza malengo baada ya kufuzu hatua ya Robo Fainali na sasa wanataka malengo mapya kuangalia uwezekano wa kuongoza kundi hilo lenye timu za Us Monastir ya Tunisia, Real Bamako ya Mali na mabingwa wa zamani wa Afrika Mazembe.

Mazembe kwa sasa ndio inayoburuza mkia wa kundi hilo ikiwa na pointi tatu, huku Yanga ikiwa kileleni na alama 10 sawa na Monastir iliyopo nafasi ya pili ambayo itamaliza mechi yake na Bamako na kama Yanga itashinda ugenini, itaongoza kundi kutegemeana na matokeo ya jijini Tunisia.

Nabi alisema Yanga ina malengo ya kushinda mchezo huo na kuweka rekodi ya kushinda ugenini, lakini kubwa ni kukwepa kuangukia kwa timu ngumu endapo itamaliza wa pili kwenye kundi hilo iwapo kama itashindwa kutoka  na matokeo mazuri ugenini mbele ya Mazembe.

“Kufuzu ni hatua moja, lakini bado tunaweza kuangalia hesabu zaidi, nafahamu haitakuwa rahisi kwa Mazembe kukubali kupoteza mchezo wa pili nyumbani, lakini tunajipanga kwenda kutafuta ushindi kule Lubumbashi,” alisema Nabi aliyeweka rekodi kubwa Yanga, na kuifanya iwe timu bora kwa kucheza soka la kuvutia.

“Sote tunafahamu kuwa kama tukimaliza nafasi ya kwanza kuna faida ya kukutana na timu za pili katika makundi mengine, lakini kama tukishindwa kupata nafasi hiyo tunaweza kuangukia kwa timu ambazo zimefanya vizuri kwenye hizi mechi sita,” alisema Nabi na kuongeza:

“Haitakuwa rahisi lakini mimi sio kocha rahisi wa kukata tamaa napenda kuishi kwa malengo nadhani kitu bora ni kujipanga na kucheza kwa hesabu sahihi.”


MASHABIKI WAPEWA MCHONGO
Wakati kocha akijipanga hivyo na timu yake huku kwingine uongozi wa timu hiyo umeamsha hamasa zaidi wakitengeneza ramani kuwasafirisha mashabiki wao tayari kwa mchezo huo.
Yanga imetoa basi  ambapo mashabiki wanaotaka kusafiri nalo watapaswa kuchangamkia fursa huku nauli ikiwa ni Sh700,000 kwa kila mtu kwenda na kurudi zikijumuisha

“Fedha hizi ni nauli ya kwenda na kurudi, vibali kama viza, kadi za manjano na vipimo vya Uviko-19 na  kwa siku tatu na kiingilio kitakuwa ni bure,” alisema ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe.