Mastaa hawa Simba ni mvua na jua

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuchambulia mastaa hao, ambao kwa sasa wanapitia kipindi kigumu wakati timu hiyo ikiwa imebakiza kuwania taji moja pekee la Ligi Kuu Bara.

KUNA mastaa wapo Simba wameonja raha na karaha, wakati timu hiyo inachukua mataji manne mfululizo, walikuwepo na ilipokosa mataji kwa mara mbili mfululizo (2021/22 na 2022/23) bado wamo.

Mwanaspoti linakuchambulia mastaa hao, ambao kwa sasa wanapitia kipindi kigumu wakati timu hiyo ikiwa imebakiza kuwania taji moja pekee la Ligi Kuu Bara.

Ingawa hadi sasa Simba ndio timu pekee yenye mataji msimu huu ikiwa nayo mawili mkononi yaani Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano, ila tayari ilishatolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho (ASFC).


AISHI MANULA - KIPA

Kipa wa Simba, Aishi Manula ameshiriki kikamilifu kwenye utawala ule wa miaka minne mfululizo yaani 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21 akicheza kwa kiwango cha juu, ingawa kwa sasa hapati nafasi kubwa kutokana na majeraha.

Mechi iliyomshusha zaidi Manula kwa msimu huu ni ile aliyofungwa na Yanga mabao 5-1 katika Dabi ya Kariakoo ya mzunguko wa kwanza, jambo lililowafanya mashabiki kupungua hamu ya kuendelea kumuona akidaka.

ALLY SALIM - KIPA

Ni kati ya makipa waliovaa medali za ubingwa ndani ya misimu minne na mechi ambazo zilimfanya aanze kuzungumzwa midomoni mwa mashabiki wake ni alipodaka dhidi ya Ihefu, Yanga na Azam FC.

Michezo mingine aliyodaka ni dhidi ya Yanga, Simba ikishinda mabao 2-0, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad timu yake ikitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3, pia kudaka kwake penalti dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii ya ufunguzi wa msimu huu, Simba ikachukua taji hilo jijini Tanga.

SHOMARI KAPOMBE - BEKI

Ni kati ya wachezaji muhimu ndani ya kikosi cha Simba na amevaa medali ya ubingwa ambao Simba ilichukua mara nne mfululizo. Kutokana na kiwango chake kuwa juu, kila kocha ajaye ndani ya kikosi hicho amekuwa akimtumia katika kikosi cha kwanza.

MOHAMED HUSSEIN 'TSHABALALA' - BEKI

Nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' ni kati ya wachezaji muhimu katika mafanikio ya ubingwa na bado anaendelea kuipambania timu hiyo, nyakati ngumu ambazo inakosa ubingwa.

MZAMIRU YASSIN - KIUNGO MKABAJI

Ni miongoni mwa viungo muhimu ndani ya Simba, alikuwepo ndani ya misimu minne ambayo timu hiyo ilichukua ubingwa mfululizo.

CLATOUS CHAMA - KIUNGO

Ana mchango mkubwa kwenye miaka minne ya ubingwa Simba, 2019/20 aliibuka mchezaji bora wa msimu, 2020/21 alimaliza na mabao manane na asisti 15 na bado anafanya vizuri ndani ya kikosi hicho.

LUIS MIQUSSIONE - WINGA

Msimu wake wa kwanza 2020/21, alinyakua taji la ubingwa na alifunga mabao tisa na asisti 10, uliofuata akauzwa Al Ahly ya Misri na amerejea tena 2023/24 timu hiyo ikiwa inasumbuka kuchukua ubingwa.

JOHN BOCCO - MSHAMBULIAJI

Ni kati ya washambuliaji waliobakia ndani ya kikosi hicho, ingawa kwa sasa haonekani uwanjani, zipo picha zikimuonyesha akiwa na timu ya vijana, alikuwa na mchango mkubwa ndani ya miaka minne Simba ikichukua ubingwa mfululizo.

Mabao aliyoyafunga Bocco katika misimu ambayo timu hiyo inanyakua ubingwa mfululizo ni 55, yaani msimu wa 2017/2018 alifunga mabao 14, 2018/2019 (mabao 16), 2019/2020 (9), 2020/2021 (16).


KENNEDY JUMA - BEKI

Japokuwa hana nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza, kwenye ubingwa wa misimu minne mfululizo, alikuwa miongoni mwao na bado yupo kikosini.