Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzuka mbio za magari sasa wahamia Iringa

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa kalenda ya chombo kinachosimamia mchezo wa mbio za magari nchini(AAT), mkoa wa Iringa utakuwa mwenyeji wa raundi ya pili katika mashindano ya siku mbili yatakayofanyika Septemba  14 na 15 mwaka huu.

MSISIMKO na mzuka wa mbio za magari umeanza  tena  baada ya klabu ya Mbio za Magari Iringa, IMSC,  kuthibitisha uenyeji wa raundi ya pili ya mbio za ubingwa wa taifa katikati ya mwezi ujao.

Kwa mujibu wa kalenda ya chombo kinachosimamia mchezo wa mbio za magari nchini(AAT), mkoa wa Iringa utakuwa mwenyeji wa raundi ya pili katika mashindano ya siku mbili yatakayofanyika Septemba  14 na 15 mwaka huu.

Hapo awali Mkoa wa Iringa ulipangwa kufungua msimu wa mbio za magari mwezi March mwaka huu, lakini mashindano hayo yaliahirishwa  baada ya mmoja  wa waasisi na wadhamini wakuu wa mchezo mkoani humo  kufariki dunia.

Baada ya kuahirishwa, msimu wa mbio za magari ulifunguliwa mjini Tanga ambako mashindano ya kilometa 155 yalifanyika mwezi Julai mwaka huu.  

“Iringa ndiyo waandaji na madereva tuko tayari kwa mchezo huu,” anasema Randeep Birdi ambaye anaongoza mbio za kusaka taji la ubingwa wa taifa baada ya kushinda raundi ya ufunguzi mjini Tanga.

Wakati macho na masikio ya  wapenzi wa mbio za magari wakimuangalia  Birdi na Gupal Sandhu aliyeshika nafasi ya pili katika mbio za ufunguzi wa msimu mkoani Tanga, anayetia homa madereva wengine ni mwenyeji Ahmed Huwel ambaye hajawahi kushindwa katika mbio za magari mkoani Iringa kwa takriban  miongo miwili sasa.

Kuwepo kwa Huwel ambaye hushiriki na gari ya kisasa aina ya  Ford Fiesta, kutatoa changamoto kwa madereva wa Mitsubishi Evo na Subaru Impreza  ambao walitamba katika mbio za ufunguzi wa msimu mkoani Tanga mwezi mmoja uliopita .

Madereva kutoka klabu za mikoa ya Arusha,Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro Morogoro  na Tanga wanategemewa kushiriki katika mashindano haya ya raundi ya pili kwa msimu huu.

Dereva na msoma ramani atakayefanya  vizuri katika raundi nyingi za mbio za magari ndiye atatwaa ubingwa wa taifa wa mwaka wa mbio za magarik kwa mujibu wa kanuni .

Katika mashindano mengi yanayofanyika mkoani Iringa, madereva kutoka Kenya, Uganda na Zambia pia wamekuwa wakishiriki  na wengi wamekuwa wakisifu ubora wa barabara na usalama wa  madereva ambavyo  pamoja na kuwepo vivutio vingi vya utalii njiani, kumezifanya mbio za magari za Iringa kuwa na mvuto mkubwa.