Mzuka huu wa wachezaji wapya Simba noma aisee

Muktasari:
- Mgosi alisema anatambua kwamba usajili bado unaendelea lakini mwanzo uliopo unawapa nguvu ya kutembea kifua mbele kujiamini kwamba wana jipya msimu ujao baada ya miaka minne kuwa wanyonge.
MCHEZAJI kiongozi wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amewaambia mashabiki wa klabu hiyo kwamba wasiwe na wasiwasi kwa mzuka waliokuja nao wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho, kitaeleweka tu msimu ujao.
Mgosi amekiri kwamba timu hiyo imeanza na kasi nzuri kwenye mazoezi na wachezaji waliosajiliwa mpaka sasa na walioko kambini Morogoro yeye anawakubali na wana vigezo vya kuchezea Simba na amewataka watu wasisikilize kejeli za Yanga.
“Tumeanza kuona mwelekeo kwenye mazoezi unaona vijana wanavyojituma wamekuwa na ushindani wa hali ya juu, tukiendelea hivi bila shaka wakati wa kicheko kile ambacho Simba, walikikumbuka umefika,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa ambaye huwa hapendi kutafuna maneno linapokuja suala la masilahi ya Simba.
Lakini alitoa angalizo moja: “Bila upendo sisi kwa sisi hata kama kuna majembe ya kufanya kazi itakuwa ngumu kufikia malengo yetu, hivyo ni wakati sahihi kwa makocha, viongozi kuwajenga wachezaji kisaikolojia ili kujitambua kwamba wao ni wanajeshi wanaotumwa kupambana vitani.”
Mgosi alisema anatambua kwamba usajili bado unaendelea lakini mwanzo uliopo unawapa nguvu ya kutembea kifua mbele kujiamini kwamba wana jipya msimu ujao baada ya miaka minne kuwa wanyonge.
“Naamini hata viongozi wanazingatia wapi ambapo walikwama na mahitaji ya wapenzi wao kwani hata wachezaji wanaotajwa kutaka kuwasajili ni wale ambao wana uwezo wa kuibeba timu,”alisema Mgosi ambaye aliwahi kuichezea FC Lupopo ya DR Congo.
Baadhi ya nyota wazawa ambao wamesaini Simba mpaka sasa ni Ramadhan ‘Shiza’ Kichuya, Mohammed Ibrahim na Mdhamiru Yasini wote kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Aveva awashangaa Yanga
Prezidaa wa Simba Tanzania, Evans Aveva ametamka kwamba Jumamosi wiki hii watampa kiungo Mzimbabwe Method Mwanjali mkataba wa mwaka mmoja mjini Morogoro kama Kocha Joseph Omog atawapa baraka zote.
Lakini Aveva akaishangaa Yanga kujihusisha na mchezaji huyo wa Caps United ya Zimbabwe.
“Nasikia mtani anataka kumsajili Mwanjali,” alisema Aveva huku akicheka ingawa baadae alisema ni utani na kusisitiza Simba iko makini katika usajili wake.
Uongozi wa Caps umekuwa ukisisitiza kwamba, Mwanjali aliwaaga kwamba anakuja Yanga na si Simba na mpaka sasa taarifa za yeye kuwa Simba wanazisikia tu kwenye magazeti ingawa hawatakuwa na kizuizi kama ameamua kubadili uelekeo.
Kwa mujibu wa Aveva, Kocha Omog amewaambia kwamba jamaa ni mashine lakini waendelee kumpa muda amcheki zaidi mpaka Jumamosi.
“Tunao wachezaji wengi kambini wanaofanya majaribio, wapo wa Congo na wengine kutoka Ivory Coast ambao wote wanasaka nafasi ya kusajiliwa pamoja na Mwanjali ambaye tunafikiria kumpa mkataba wa mwaka mmoja.
“Jumamosi mimi mwenyewe nitakwenda Morogoro kushuhudia mwenendo wa kambi kwa mara nyingine tena, baada ya Jumamosi ndipo tutafanya mchakato wa kumsainisha Mwanjali na nitaeleza zaidi nini kinaendelea,” alisema Aveva.
“Tumedhamiria kurejesha hadhi ya soka ya Simba, sanjari na kujipanga kwa vyovyote vile kutwaa ubingwa msimu ujao, ndiyo sababu tunataka kufanya usajili wa nguvu ili kutimiza dhamira hiyo,” alisisitiza bosi huyo wa Simba.
“Hili ni zoezi endelevu, msimu huu hatutaki kukosa taji, tunafanya usajili kulingana na matakwa ya kocha Omog (Joseph) na benchi lake la ufundi,” alisema Aveva.
Mzimbabwe huyo amewahi kuwa nahodha wa timu yake ya taifa iliyotwaa ubingwa wa Cosafa mwaka 2009, amewahi kuichezea, Mamelody Sundowns na Mpumalanga Black Access za Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Katika hatua nyingine, mashabiki wa Simba wameanza mikakati ya kuhakikisha wanaisapoti timu yao na tayari wamefanya kikao kwa ajili ya kupanga bajeti ya kusafiri na timu hiyo katika kila mechi itakayokwenda kucheza ugenini.
Katibu wa kundi la ushangiliaji la Simba maarufu kama Wekundu wa Terminal, Joel Mwakitalima aliliambia gazeti hili jana kwamba wameanza mikakati hiyo ambayo pamoja na mambo mengine ni kuanza kuandaa bajeti ya kundi kwa ajili ya safari za mikoani.
“Tunajiamini na tunaamini timu yetu itafanya vizuri msimu ujao kutokana na juhudi za kuimarisha kikosi zinazofanywa na uongozi wetu, sisi tuko nao pamoja kama mchezaji wa 12 na popote itakapokwenda Simba tutaambatana nayo kwa ajili ya kuipa sapoti, achilia mbali mechi za Taifa msimu ujao,” alisema Mwakitalima.