Prime
Mzize aitaka Ulaya, awakataa Waarabu

Muktasari:
- Mzize ambaye amekuwa na mwendelezo mzuri tangu ajiunge na Yanga kutoka timu ya vijana, nyota huyo amekuwa akitolewa macho na klabu za nje zinazoitaka saini yake, lakini mwenyewe akidaiwa kusema ataweka kila kitu chake hadharani, ila kwa sasa anapambana kuipa Yanga mataji inayotetea.
DILI kibao zimetua mezani kwa mabosi wa Yanga kutoka timu zinazotaka kumsajili mshambuliaji Clement Mzize zikiwamo kutoka Afrika Kaskazini, Saudia Arabia na Ulaya, lakini straika huyo mwenye mabao 13 kwa sasa Ligi Kuu Bara amezichomolea za Kiarabu, huku ikielezwa hesabu zake ni kutaka kucheza Ulaya.
Mzize ambaye amekuwa na mwendelezo mzuri tangu ajiunge na Yanga kutoka timu ya vijana, nyota huyo amekuwa akitolewa macho na klabu za nje zinazoitaka saini yake, lakini mwenyewe akidaiwa kusema ataweka kila kitu chake hadharani, ila kwa sasa anapambana kuipa Yanga mataji inayotetea.
Ofa ya awali ambayo Yanga iliichomoa ilikuwa ni ya Wydad Casablanca ya Morocco na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kabla ya klabu moja ya Saudi Arabia na nyingine ya barani Ulaya zinazomtaka Mzize.
Hivi karibuni ikaelezwa kuwa klabu mbili za Ufaransa za Olympique Lyonnais na AS Saint-Etienne zinazoshiriki Ligue 1 zinadaiwa zimeonyesha nia ya kumtaka mchezaji huyo mbali na klabu moja ya Ubelgiji na kuwafanya mabosi wa Jangwani kukuna vichwa wakipima uzito wa mzigo watakaopewa.
Hata hivyo, inaelezwa Mzize amewaambia mabosi wanaomsimamia kwamba anataka kwenda kucheza Ulaya na ishu za timu za Uarabuni hana mpango nazo.
Inaelezwa kwamba ofa zilizowekwa na timu za Ulaya ni kubwa na zilizomvutia mchezaji huyo tofauti na klabu za Afrika Kaskazini au Saudia Arabia.
Mwanaspoti liliwahi kuripoti kuwa, Wydad iliyokuwa imefika dau la Dola 1 milioni kabla ya USM Alger kutuma ofa ya Sh1.8 bilioni, lakini Klabu ya Yanga ikazigomea ikitaka ziongeze zaidi na ndipo zikaibuka dili za klabu za Ubelgiji na Ufaransa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Alfred Raul ambaye ni skauti wa klabu za Ubelgiji, alisema kama dili hizo zilizopo mezani zitatiki, basi Mzize atakuwa amekula shavu kubwa.
“Kweli kuna klabu kubwa mbili za hapa Ubelgiji, tunazizungumzia timu ambazo zinacheza Ligi Kuu ya hapa zote zimenipa kazi ya kuwatafutia huyu Clement (Mzize). Ni mchezaji mdogo mwenye nishati kubwa. Nadhani Tanzania itanufaika akija Ubelgiji, kwani atakuwa katika nafasi kubwa ya kuonekana.
“Tumeanza kuwatafuta wasimamizi wake nadhani tunakwenda vizuri tutafika hadi kwa uongozi wa klabu yake kutengemea na namna wasimamizi wake watakavyotueleza juu ya mkataba wake,” alisema skauti huyo huku akigoma kutaja majina ya timu hizo.
Taarifa nyingine zilizowahi kuthibitishwa na Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ni kwamba Mzize anatakiwa na klabu za Ufaransa, na inaelezwa ofa hizo za Ulaya ndizo anazozitaka zaidi nyota huyo.
Mzize ambaye rekodi zake zinapanda kila msimu, uwezo wake umezivutia klabu nyingi, lakini kubwa kuliko ni idadi inazidi kuongezeka.
Yanga imemsainisha Mzize mkataba mpya kimyakimya unaomfanya aendelea kusalia ndani ya klabu hiyo kwa miaka miwili zaidi hadi mwaka 2027.
Inaelezwa menejimenti ya mchezaji huyo inapambana kuhakikisha wanamtafutia Mzize timu itakayompa manufaa makubwa katika maisha yake, hasa maslahi binafsi na kumfungulia milango ya kuonekana zaidi Ulaya.
Rekodi za Mzize zinaonyesha katika msimu wa kwanza 2022-2023, alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu, ambapo mbali na hilo ila alichangia upatikanaji wa mabao sita, akifunga matano na kuasisti moja kati ya 61 ya timu nzima.
Msimu huo, Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kukosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria kufuatia sare ya jumla ya mabao 2-2, ikichapwa nyumbani 2-1, kisha ugenini kushinda 1-0.
Msimu wa pili wa 2023-2024, Mzize alichangia mabao 13, baada ya kufunga sita na kuasisti saba kati ya 71 ya kikosi hicho kizima, kilichotwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara ukiwa ni wa tatu mfululizo kufuatia kukusanya pointi zake 80, lakini akifunga pia mabao matano katika Kombe la Shirikisho (FA).
Katika huu ndio ukawa bora zaidi kwa mshambuliaji huyo, kwani hadi sasa amechangia mabao 16 ya Ligi Kuu Bara kati ya 68 yaliyofungwa na kikosi kizima n kukusanya pointi 70, baada ya kucheza mechi 26. Mzize amefunga mabao 13 na kuasisti matatu akishika nafasi ya pili nyuma ya Jean Ahoua wa Simba aliyefunga 15 baada ya juzi kupiga hat trick, walipoizamisha Pamba Jiji kwa mabao 5-1.