JKT yachemsha Bara, ila kazi ipo huku

Muktasari:
- JKT inayoshika nafasi ya saba kwa sasa imesaliwa na mechi tatu za kukamilisha msimu, lakini ikiwa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), ikijiandaa kukabiliana na Yanga Mei 18, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
MAAFANDE wa JKT Tanzania kupitia kocha mkuu, Ahmad Ally wamekiri wamechemsha kwa kushindwa kufikia malengo ya Ligi Kuu ya kumaliza ndani ya 5-Bora, lakini kilichobaki kwa sasa wanaelekeza nguvu zote katika Kombe la Shirikisho (FA) ili wakate tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
JKT inayoshika nafasi ya saba kwa sasa imesaliwa na mechi tatu za kukamilisha msimu, lakini ikiwa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), ikijiandaa kukabiliana na Yanga Mei 18, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
JKT Tanzania imetinga hatua hiyo kwa kuing’oa Pamba Jiji kwa mabao 3-0 zilipokutana robo fainali, wakati Yanga iliinyoosha Stand United ‘Chama la Wana’ kwa mabao 8-1.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ahmad alisema malengo yao yalikuwa ni kumaliza katika nafasi tano ya ligi, lakini kutokana na kudondosha pointi nyingi hasa duru la pili imewafelisha na haioni nafasi hiyo tena kwa vile timu zilizopo juu yao Azam, Singida BS, Tabora Utd na Dodoma Jiji zimewazidi ujanja.
“Akili, nguvu na jitihada zetu kwa sasa tumewekeza katika mechi ya nusu fainali ya Shirikisho (FA) dhidi ya Yanga ili kuona tunaenda fainali na kujiweka pazuri kubeba ubingwa na kupata tiketi ya CAF baada ya kukwama katika Ligi Kuu Bara,” alisema Ahmad na kuongeza;
“Tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano haya na kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa hivyo tunawekeza nguvu huku ili kuwa katika nafasi nzuri, tunaamini haitakuwa rahisi kwasababu tunakutana na timu ambayo tuliizuia kwenye mchezo wa ligi.”
Ahmad alisema mechi tatu za ligi zilizobaki mikakati ni kupata matokeo bila kudondosha pointi lakini bado haoni wakifikia malengo yao hivyo wameamua kuwekeza nguvu zaidi FA ili wapate tiketi ya uwakilishi kimataifa.
“Tunaifahamu Yanga ni timu hatari kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji lakini naamini sisi pia tupo imara na tunapenda kucheza mechi kubwa tupo tayari kwa ushindani na matarajio ni kutinga hatua inayofuata.”