Tiketi ya CAF yampa presha kocha Azam FC

Muktasari:
- Azam, iliyong’olewa mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliyoshiriki msimu huu ikiwa ni mara yake ya pili baada ya kuicheza mwaka 2015, lakini haipo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara wala Kombe la Shirikisho (FA) ilikotolewa raundi ya 32 na Mbeya City.
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema matokeo mabaya iliyopata timu hiyo katika mechi za hivi karibuni za Ligi Kuu Bara ni moja ya sababu za kuwarejesha haraka kambini wachezaji ili kujiandaa na mechi tatu za kufungia msimu zitakazoamua hatma yao ya CAF.
Azam, iliyong’olewa mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliyoshiriki msimu huu ikiwa ni mara yake ya pili baada ya kuicheza mwaka 2015, lakini haipo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara wala Kombe la Shirikisho (FA) ilikotolewa raundi ya 32 na Mbeya City.
Jambo hilo limeifanya timu hiyo kusaliwa na tumaini pekee la kukata tiketi ya CAF kwa msimu ujao kwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu inayoiwania na Singida Black Stars, jambo linalompa presha kocha Taoussi aliyesema amewaita mapema kambili wachezaji na kuzungumza nao juu ya kufanya kila linalowezekana kumaliza vyema mechi zilizosalia.
Azam imekabiza mecchi tatu dhidi ya Dodoma jiji iliyopangwa kupigwa Mei 13, kabla ya kuvaana na Tabora United na kumalizana na Fountain Gate zitakazopigwa kati ya Juni 18 na 22 kuhitimisha msimu, huku ikisikilizia pia matokeo ya Singida ambayo ipo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).
Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema hawajatimiza lengo hata moja msimu huu katika michuano waliyoshiriki, hivyo kilichobaki ni kutumia vizuri dakika 270 ili waweze kukusanya pointi tisa zitakazowafanya waendele kusalia katika nafasi ya tatu, huku wakiiombea mabaya Singida iliyopo nyuma yao.
Singida imebakiza mechi nne ikiwamo kiporo dhidi ya Simba na kama ikishinda zote itavuna pointi 12 ambazo ukijumlisha na 53 ilizonazo zitaifanya ifikishe 65, mbili zaidi ya zinazoweza kufikiwa na Azam yenye 54 kwa sasa, ambayo ina mechi tatu mkononi na ikizishinda itafikisha pointi 63 tu.
“Ni kweli hatuna matokeo mazuri baada ya kuenguliwa katika mataji yote tuliyowania msimu huu, nimewaita vijana wangu kambini haraka ili kujiweka tayari kwa mechi tatu zilizobaki. Haitakuwa rahisi, ila mipango inaendelea kusukwa na wachezaji wanatambua kazi tuliyonayo,” alisema Taoussi na kuongeza;
“Wapinzani wanaotufukuzia nafasi ya tatu tumewaacha kwa pointi moja hii sio nzuri kwetu licha ya kuanza kwa ushindani mzunguko wa pili tumedondosha pointi nyingi na ndio wa lala salama hivyo mikakati ni kuhakikisha hatudondoshi pointi hata moja kwenye mechi tatu zilizobaki japo haitakuwa rahisi.”
Taoussi alisema katika mechi tano zilizopita za ligi wamepoteza pointi sita wakifungwa mechi mbili na kukusanya tisa baada ya kushinda tatu wanahitaji matokeo mechi tatu ili kuwa na mwendelezo wa mechi nne mfululizo kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ushiriki kimataifa Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ni ligi tu ndio itatupa uwakilishi Shirikisho hivyo tunahitaji kuwekeza nguvu zaidi ili tupate uwakilishi huo wachezaji wanatambua umuhimu wa kupata matokeo kwenye michezo hiyo mitatu na tumekaa na kupanga mikakati njia gani tunafaa kupita ili tufikie malengo.”