Prime
Mzimu wa RS Berkane bado mtihani kwa Fadlu

Muktasari:
- Ni baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya RS Berkane kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa kimataifa wa Godswill Akpabio, Nigeria, baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120.
MIAKA mitatu iliyopita, Fadlu Davids alipitia moja ya siku zenye maumivu kwenye taaluma yake ya ukocha. Mei 20, 2022, akiwa msaidizi wa Mandla Ncikazi katika kikosi cha Orlando Pirates, aliishuhudia ndoto ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika ikiyeyuka.
Ni baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya RS Berkane kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa kimataifa wa Godswill Akpabio, Nigeria, baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120.
Sasa, miaka mitatu baadaye, hatimaye imemrudisha Fadlu katika ulingo ule ule wa ndoto, safari hii si kama msaidizi, bali ni kocha mkuu wa Simba SC. Bahati iliyoje anakutana na mpinzani yule yule, RS Berkane. Hili si jambo la kawaida, ni kama hadithi inayohitaji kuandikwa upya.
Akizungumza kwa utulivu lakini kwa sauti nzito inayobeba hisia za safari yake, Fadlu alisema: “Soka linatupa nafasi ya pili, jambo ambalo si wote hulipata. Najua maumivu ya kupoteza mbele ya RS Berkane, najua hisia za kuanguka hatua moja kabla ya taji. “Safari hii nipo Simba, nipo tayari kupambana hadi mwisho kwa ajili ya historia yetu na heshima ya mashabiki wetu.
“Tunawaheshimu RS Berkane kwa uzoefu na ubora wao, lakini tutajipanga kupambana kwa dakika 90, 120 au hata mikwaju ya penalti kama itahitajika. Lengo letu ni moja tu kwa sasa kushinda ubingwa wa Afrika.”
Fadlu amesisitiza katika kipindi cha maandalizi kuelekea kuikabili RS Berkane, atawaandaa vijana wake kucheza kwa kasi na umakini mkubwa baada ya kugundua wapinzani wao ni hatari kwenye kushambulia kwa kasi, pia wanalinda vizuri lango lao.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, hataki kuona yanajirudia ya mara ya mwisho kucheza dhidi ya Berkane, hivyo katika mazoezi yake programu ya kupiga penalti itakuwepo.
Simba SC imeandika historia mpya msimu huu kwa kufuzu fainali ya CAF baada ya miaka 32 kwa bao 1-0 dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini.
Kwa upande wa RS Berkane, nao wamethibitisha si timu ya kubeza. Kwa kuwatoa CS Constantine ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1, Wamorocco hao wamesisitiza uzoefu wao mkubwa katika michuano ya CAF bado ni silaha kubwa wanayokuja nayo katika fainali dhidi ya Simba.
Simba na RS Berkane si wageni kwa kila mmoja. Msimu wa 2021/22, walikutana hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mchezo wa kwanza uliopigwa Morocco, Simba walipoteza mabao 2-0, lakini walijibu nyumbani kwa ushindi wa bao 1-0 la Pape Ousmane Sakho.
Katika kundi lao, wote walikusanya pointi 10, lakini RS Berkane walimaliza vinara kwa tofauti ya mabao. Simba waliishia hatua ya robo fainali walipokutana na Orlando Pirates na kuondolewa kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 1-1 safari ambayo Fadlu alikuwa sehemu ya mafanikio ya Pirates kwa wakati huo.
Berkane waliendeleza moto wao kwa kuitoa Al Masry kwa faida ya mabao ya ugenini, kisha wakaiondosha TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-2 kwenye nusu fainali, kabla ya kuikabili Orlando Pirates katika fainali. Napo ndipo walipoandika huzuni ya Fadlu, wakibeba taji kwa penalti.
Kwa Fadlu mchezo huu wa fainali una maana kubwa zaidi ya taji. Ni nafasi ya kusafisha kumbukumbu ya machungu ya 2022, ni nafasi ya kuthibitisha ukuu wake kama kocha mkuu mwenye uwezo wa kubadilisha ndoto kuwa halisi.