Mzimu wa 2003 kuinusuru Simba jijini Cairo

mshambuliaji mpya wa simba, Boban
SIMBA inahitaji kukumbuka mafanikio yake ya mwaka 2003 iliyoyapata jijini Cairo ilipoifunga Zamalek bao 1-0 ,wakati itakaposhuka dimbani Mei 28 kuikabili Wydad Casablanca kwenye mchezo mmoja wa kuwania kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana lilitangaza ratiba ya mechi hiyo kati ya Wydad Casablanca ya Morocco na Simba kuchezwa kwenye Uwanja wa Petrosport jijini Cairo, Misri baada ya Simba kushinda rufaa yao dhidi ya mabingwa watetezi TP Mazembe kwa waliomchezesha mchezaji ambaye hakuwa na leseni. Simba inayo kumbukumbu ya kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi katika mashindano hayo baada ya kuitoa Zamalek kwa kuifunga bao 1-0 katika mechi zote mbili. Ushindi wa kwanza ilioupata jijini Cairo dhidi ya Zamalek ndio ulikuwa wa pekee kwao kupata ugenini dhidi ya klabu za Afrika Kaskazini. Lakini mwaka jana ilipokea kipigo cha mabao 5-1 jijini Cairo na Haras El Hodoud. Historia ya mafanikio ya Simba dhidi ya timu za nchi za Kiarabu imeyapata zaidi ikiwa inacheza na timu hizo nchini Tanzania kwenye uwanja wake wa nyumbani. Mwaka 1974, iliichapa Mehara El Kubra ya Misri bao 1-0 kwenye nusu fainali ya Club Championship, miaka tisa baadaye iliinyuka Al Ahly 2-1 jijini Mwanza katika Kombe la Washindi kabla ya kuichakaza Al Arach ya Algeria kwa mabao 3-0 kwenye robo fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993. Mwaka1995, timu ya Misri ya Arab Contractors ilipokea kipigo kutoka kwa Simba cha mabao 3-1, miaka sita baadaye Al Ismail ilifungwa 1-0 na Simba kabla ya mechi kuvunjika kutokana na mvua kubwa, iliporudiwa kesho yake Ismail ililazimisha sare na baadaye 2003 Simba walifuzu kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuitoa Zamalek. Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, mechi hiyo ya Simba dhidi ya Wydad Casablanca itakuwa kama fainali kwani endapo timu hizo zitashindwa kufungana kwenye muda wa kawaida wa dakika 90, basi mshindi atapatikana kwa changamoto ya mikwaju ya penalti. Wenyeji wa mechi (kwa maana ya kupokea timu na viongozi uwanja wa ndege) ni Chama cha Mpira wa Miguu cha Misri (EFA). Gharama nyingine zozote zitabebwa na timu husika kupitia vyama vyao-Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Morocco (FRMF). Kila timu itajigharamia usafiri wa kwenda Cairo, pamoja na gharama za malazi. EFA imeombwa kusaidia timu zote katika maandalizi ya hoteli za kufikia. Gharama za maofisa wa mchezo (waamuzi na kamishna) ikiwemo usafiri na malazi zitabebwa na klabu hizo kupitia vyama vyao (TFF na FRMF). Gharama zozote ambazo EFA itatumia katika maandalizi ya mechi hiyo zitarejeshwa na TFF na FRMF. Mwenyekiti wa Simba, Ismaili Aden Rage alisema kuwa kwa upande wao wamejiandaa na mchezo huo na wamepanga kuondoka nchini kwenda Misri siku ya Jumatano. Alisema Simba ni timu ya wananchi na sasa wameirudisha kwa wanachama baada ya kutoka mikononi mwa watu hivyo wako tayari kwa gharama zozote baada ya CAF kudai kuwa timu hizo zitajigharamia usafiri na malazi. Hata hivyo CAF imesema mapato yatakayopatikana kutokana na viingilio katika mechi hiyo, itayagawa nusu kwa nusu kwa klabu hizo kupitia vyama vyao vya mpira wa miguu. Rage alisema wanajua fitina za Wamisri ni kali sana, lakini nao wanajipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kuingia hatua ya makundi. Timu itakayoshinda itaingia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ambayo itachezwa kwa mtindo wa Ligi nyumbani na ugenini ili kuwania kucheza nusu fainali. Simba ikishinda itakuwa kundi B pamoja na Al Ahly ya Misri, Esperence (Tunisia) na Moloudia Club d’Alger ya Algeria. MASHABIKI Mashabiki wa Simba jana walifurika uwanjani kushuhudia mazoezi ya timu yao yaliyokuwa yakiendelea kwenye Uwanja wa Taifa. Mashabiki hao walikuwa wakipiga kelele za kutaka viongozi wao wajenge uwanja wao kwa madai ya kuchoka kunyanyaswa baada ya kuwazuia kwa muda kuingia uwanjani humo hadi pale walipojaribu kuvunja geti na kuingia. "Tupo tayari kulipa hata 'buku' Sh 1000 ili kuangalia mazoezi, lakini si kufanyiwa hivi. Mazoezi hayo yalipambwa na uwepo wa nyota wote wa Simba wakiwemo Haruna Moshi 'Boban', Hillary Echessa, huku kipa wa zamani wa timu hiyo Idd Pazi 'Father' akitoa mazoezi kwa makipa Juma Kaseja na Ally Mustapha.