Mzambia Yanga afanya maamuzi magumu
Muktasari:
- Yanga iliyoondoka kwa Ndege ya Shirika la Emirates ikiwa na msafara wa nyota 18 tayari kwa mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi usiku mjini Algiers, imewaacha mabeki Vincent Bossou na Oscar Joshua kwa maelekezo ya Lwandamina.
KIKOSI cha Yanga kiliondoka nchini jioni ya jana Alhamisi kuelekea Algeria kwa ajili ya pambano lao la marudiano la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger, lakini Kocha Mkuu wake, George Lwandamina, akaamua kufanya maamuzi magumu.
Mzambia huyo amewakata mabeki wake wawili katika dakika za mwishoni kabla ya safari, lakini hapo hapo taharuki ya mgomo ndani ya kikosi hicho ikamalizwa na Mwenyekiti wao, Yusuf Manji, aliyewaibukia mazoezini Uwanja wa Taifa.
Yanga iliyoondoka kwa Ndege ya Shirika la Emirates ikiwa na msafara wa nyota 18 tayari kwa mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi usiku mjini Algiers, imewaacha mabeki Vincent Bossou na Oscar Joshua kwa maelekezo ya Lwandamina.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba Bossou ameondolewa baada ya juzi kudai hataweza kucheza mchezo huo kutokana na maumivu ya mguu, ingawa kocha alipokea sababu hiyo kwa shingo upande.
Katika mazoezi ya juzi Uwanja wa Taifa, Bossou hakushiriki mazoezi hayo alikuwa nje sambamba na Thabani Kamusoko, Donald Ngoma waliosafiri na Obrey Chirwa ambaye aligoma mapema akishinikiza kulipwa mishahara yake ya miezi miwili.
Oscar naye aliachwa kutokana na maelekezo ya kocha huyo, licha ya kufanya mazoezi vizuri.
Manji alainisha wachezaji
Katika mazoezi hayo ya juzi gumzo lilikuwa ni kitendo cha Yusuf Manji kwa mara ya kwanza tangu atoke katika matatizo yake kuwaibukia wachezaji na kuteta nao kwa usiri kubwa akituliza mgomo uliokuwa ukifukuta.