Mwenye Yanga yake kaja sasa

MKALI WA MECHI ZA KIMATAIFA: Baada ya kuipa Zesco ubingwa kwa misimu miwili mfululizo, kocha huyu aliiongoza timu hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016.
Muktasari:
- Lakini sasa picha linaendelea. Lwandamina anarudi Dar es Salaam keshokutwa Jumapili mchana tayari kusaini mkataba na kuanza kazi Jangwani wiki ijayo jambo ambalo linamaanisha ndani ya saa 48 zijazo huenda Pluijm hatakuwa kocha wa Yanga. Huenda pia asiwe Mkurugenzi wa ufundi kama viongozi walivyokuwa wamefikiria awali kwavile wamebadili mawazo.
KOCHA Mzambia, George Lwandamina alitua Dar es Salaam kimyakimya Oktoba 23 kwaajili ya kumalizana na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji. Lakini Mwanaspoti likamnasa kwenye Uwanja wa Ndege na kumwaga picha zake kwenye ukurasa wa mbele wa siku iliyofuata.
Tukio ambalo Yanga lilimshtua kocha wa Yanga, Hans Pluijm ambaye aligundua kwamba viongozi wanamzuga akaamua kutangaza kujiuzulu jioni ya Oktoba 24. Viongozi wa Yanga wakaendelea kuzuga kwa kumkana Lwandamina kwa nguvu zote na wakamwambia awazuge watu kwamba amekuja kwa ishu zake.
Baadae Yanga wakamtumia shabiki wao maarufu ambaye kikazi ni Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba kumshawishi Pluijm abadili uamuzi wake na kweli akakubali kuendelea na Yanga.
Lakini sasa picha linaendelea. Lwandamina anarudi Dar es Salaam keshokutwa Jumapili mchana tayari kusaini mkataba na kuanza kazi Jangwani wiki ijayo jambo ambalo linamaanisha ndani ya saa 48 zijazo huenda Pluijm hatakuwa kocha wa Yanga. Huenda pia asiwe Mkurugenzi wa ufundi kama viongozi walivyokuwa wamefikiria awali kwavile wamebadili mawazo.
Kocha huyo ambaye ameshaachana na Zesco ya Zambia, akitua tu Jumapili atasaini mkataba wa miaka miwili. Habari za ndani zinadai kwamba baada hali kuchafuka juzi, jana mabosi wa Yanga walikuwa wakihaha kuhakikisha anarudi nchini haraka hata kwa ndege za kuunganisha kutoka mji wa Ndola kufika Lusaka mpaka Dar es Salaam.
Awali ilikuwa atue leo Ijumaa mchana, lakini amekumbwa na tatizo la mwanae kutiwa mbaroni, hivyo kuomba abadilishiwe tiketi ili aje keshokutwa kabla hata Yanga haijaumana na Prisons kwani anataka kuona mechi za nje ya Dar es Salaam zinakuwaje.
Ingawa ujio wake unaweza kumpagawisha Pluijm na akatangaza tena ghafla kujiuzulu kabla hajapewa barua, habari zinadai kwamba Lwandamina alipanga kuanza kazi kwenye mechi na Ruvu Shooting katika Uwanja wa Uhuru.
Tayari Mwanaspoti linafahamu kwamba kuja kwa Lwandamina kutafuatiwa na wasaidizi wake wawili ambao nao ni kutoka nje ambao ni kocha msaidizi wa kwanza na daktari wa viungo.
Lakini zali la aina yake huenda likamuangukia kocha wa makipa, Juma Pondamali ambaye mpaka sasa hana mkataba. Mchezaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua anapewa nafasi kubwa ya kuwa meneja ingawa watu wake wa karibu wanadai kwamba anasita sana kuacha kazi yake ya muajiri wa sasa ambaye ni Serikali.
Kocha Boniface Mkwassa ndiye alikuwa akipewa nafasi ya kuwa msaidizi lakini upepo unaonekana kubadilika baada ya yeye kuwaambia Yanga kwamba anataka kuwa bosi mkuu, lakini vilevile hata Lwandaminda amewaambia Yanga wakaushe tu atakuja na mtu wake.
Katika hatua nyingine, Yanga wanajilaumu kwa kukosa Sh 5 milioni kwa kipigo hicho.
Taaarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba mabosi wa Kamati ya Mashindano waliwahojiwa wanafikiri ni idadi gani ya mabao wataifunga Mbeya City na wao kutamka kwamba watapiga mtu bao tano lakini mambo yakawageukia na wakaambulia kichapo cha maana.