Mwenye namba amerudi Simba

SIMBA jana Jumatatu ilirudi nchini ikitokea Ndola Zambia baada ya kucheza mechi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos na kupata sare ya mabao 2-2, lakini kubwa zaidi ni kurejea kwa kipa wake namba moja, Aishi Manula.

Manula aliumia nyonga Aprili 7, mwaka huu kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) dhidi ya Ihefu, jeraha lililosababisha kufanyiwa upausaji na kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.

Mwanzoni mwa mwezi huu, kipa huyo alianza mazoezi ya viungo, gym na yale ya kisayansi na kuimarika kidogokidogo na wiki hii atafanyiwa vipimo vya mwisho kujua maendeleo yake kisha baada ya hapo ataruhusiwa kujiunga na timu kwa ajili ya mazoezi ya jumla na utakuwa uamuzi wa Kocha Robertinho kama amtumie au hapana.

Wakati Manula akiwa majeraha, Simba ilihaha kutafuta mrithi wake ndipo ikamsajili Mbrazil, Jefferson Luiz ambaye alipata majeraha wakati timu ikiwa kwenye maandalizi ya msimu huu Uturuki na kuachana naye kisha ikamsajili Ayoub Lakred kutoka Morocco sambamba na Hussein Abel kutoka KMC walioingia kikosini kuongeza nguvu kwa Ally Salim na Feruz Teru lakini wote wanaonekana kutokuwa na viwango sahihi.

Hata hivyo, Salim ndiye aliyepata nafasi kubwa ya kucheza lakini bado hakufikia ubora wa Manula na hata Ayoub alipopewa nafasi kwenye mchezo dhidi ya Dynamos alifanya makosa ambayo yaliwafanya mashabiki wa Simba kumkumbuka Manula.

Daktari wa Simba Edwin Kagabo akizungumza na Mwanaspoti alisema hali ya Manula inaendelea vizuri na amekuwa akifanya kwa usahihi programu anazopewa na muda wowote anaweza kujiunga na wenzake.

“Alipewa mazoezi tiba na kuyafanya vizuri, ameimarika kwa haraka sana na baada ya vipimo vya mwisho baada ya timu kutua anaweza kujiunga na wenzake,” alisema Kagabo.

Kwa maana hiyo kama Manula ataanza mazoezi wiki hii, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kikosini kwenye mechi ya kwanza ya African Super League dhidi ya Al Ahly kutoka Misri mchezo utakaopigwa Oktoba 20, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa.