Mwandishi wa Mwanaspoti aibuka mwandishi bora wa Ligi Daraja la tatu Mwanza

Mwandishi wa kampuni ya Mwananchi, Damian Masyenene (Wa kwanza kulia) akipokea tuzo ya mwandishi bora wa Ligi Daraja la Tatu (Gazeti) kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (wa tatu kulia). Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
- Ligi hiyo ilianza Novemba 25 mwaka jana ikianza hatua ya awali na baadae nane bora huku Wilaya ya Sengerema ikikosa wawakilishi
Mwakilishi Kampuni ya Mwananchi Communications Limited inayozalisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen mkoa wa Mwanza, Damian Masyenene ametunukiwa tuzo ya Mwandishi Bora wa michezo upande wa magazeti katika mashindano ya Ligi ya mkoa wa Mwanza.
Masyenene ametunukiwa tuzo hiyo leo katika hafla ya kukabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi wa mashindano ya Ligi daraja la tatu mkoa wa huo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Washindi wengine waliokabidhiwa tuzo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi ni Alexander Sanga (mpiga picha bora), Rashid Ratto (mwandishi wa Redio) na Abdallah Chausi (Mwandishi Bora wa Mtandao).
Hafla hiyo ilinogeshwa na mchezo maalum uliozikutanisha Mapinduzi FC (bingwa mpya) dhidi ya Copco Veteran (bingwa wa zamani) inayoshiriki First League (zamani daraja la pili) ukimalizika kwa suluhu (0-0).
Mchezaji Antony Paul wa OAU FC amekuwa mchezaji bora, Kelvin kamalamo wa Mapinduzi akiibuka Kipa bora, Iddy Kasongi (Mafia FC) amekuwa mchezaji Chipukizi huku Mussa Magogo wa Mapinduzi FC akishinda kuwa kocha bora wa mashindano hayo.
Timu ya Mapinduzi (Nyamagana) imebuka bingwa kwa pointi 16, OAU FC ya Nyamagana ikimaliza na pointi 12 nafasi ya tatu ikikamatwa na Stand Express ya wilayani Misungwi.
Mshindi wa tatu (Stand Express) na mshindi wa pili (OAU) wamepata Sh 300,000 kila mmoja huku bingwa wa msimu huu Mapinduzi FC wakizawadiwa Sh 1 Milioni na kikombe.