Mwamnyeto, Kaseke kuikosa Kagera

Wednesday September 29 2021
mwamnyeto pic
By Charity James

Kocha mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema anatarajia kumkosa beki wake kisiki Bakari Mwamnyeto kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar kesho.

Mbali na Mwamnyeto Yanga watamkosa pia Deus Kaseke wote walipata shida kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Nyota wengine watakaokosekana ni Mukoko Tonombe, Dickson Ambundo, Yassin Mustafa, Saido Ntibazonkiza ambao wamewaacha Dar es Salaam chini ya uangalizi wa kocha wa viungo.

Pia kwa wachezaji waliosafiri nao wanatarajia kumkosa Deus Kaseke na Bakari Mwamnyeto ambaye aliumia kwenye mchezo dhidi ya Simba ambao walipata ushindi wa bao 1-0 na kutwaa ngao ya jamii.

“Tumepata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki na tunaimani hii ni kutokana na ukubwa wa timu ambayo imekuwa na mashabiki nchi nzima  hivyo hawajashangazwa na mapokezi wanaahidi ushindi ili kuwapa furaha,” anasema.

“Morali ya wachezaji iko vizuri na wachezaji wanafahamu wanakutana na timu ya aina gani? Kuhusu uwanja hawana sababu ya kulalamikia uwanja wa nyasi bandia lengo lao ni kukusanya pointi tatu kwenye kila mchezo ata wakicheza kwenye uwanja wa vumbi,” alisema Nabi.

Advertisement


YANGA YAANZA TIZI

Kikosi cha Yanga kimeanza mazoezi saa 10:00 jioni huku kocha   Nabi akiwa makini kuwapanga vyema vijana wake mazoezini, kukwepa mbinu za kocha Francis Baraza ambaye amemtajia kuwa ni bora.

Yanga imeendelea na mazoezi ya kibabe kuelekea mchezo huo, lakini Nabi katika kuhakikisha vijana wake wanatambua jinsi ya kuzingatia maelekezo yake amekuwa akiwataja ubora wa wapinzani na umuhimu wa mchezo wao kesho.

Kocha Nabi ameonekana kukomaa na nidhamu ya ukabaji ambapo amekuwa akiwapa mbinu mabeki wake wa pembeni mbinu za kuwazuia wapinzani wao.

Sambamba na hilo, Nabi amekuwa akiwapa akili ya jinsi ya kuwazuia viungo hao huku wachezaji hao hasa mabeki wa pembeni nao wakipambana kurekebisha.


ANATAKA MABAO

Mbali na mabeki hao pia Nabi alikuwa akikomaa na washambuliaji wake ambapo kila walipofika eneo la hatari alitaka kuona mabao yanafungwa lakini viungo nao wanatoa pasi zilizo sahihi.

Eneo hilo alikuwa akitaka kuona kila mshambuliaji anakuwa na utulivu katika kutumia nafasi ambapo eneo la kiungo pia akitaka kuona pasi za haraka zinapigwa kuweza kukamilisha mashambulizi.

Kuonyesha kocha huyo raia wa Tunisia anataka usikivu ili ufanisi upatikane, nusura atibuane na Ditram Nchimbi ambaye alikuwa akiongea na wenzake wakati kocha huyo akitoa maelekezo.


MASHABIKI WAZUIWA


Mashabiki wa Yanga wamezuiliwa kuingia kwenye uwanja wa Kaitaba kushihudia timu yao ikijiandaa na mchezo wa Ligi dhidi ya Kagera Sugar kesho.

Yanga inafanya maandalizi yake ya meisho kuwakabiri Kagera Sugar kwenye mchezo wao wa kwanza baada ya kufunguliwa rasmi jana kwa mechi tatu kuchezwa.

Mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo wameishia kuchungulia kwenye baadhi ya matundu yaliyopo kwenye kuta zinazouzunguka uwanja wa Kaitaba.

Mmoja wa mashabiki waliojitokeza aliyefahamika kwa majina ya Ramadhan Said anasema “wamesikitishwa na kitendo cha kuzuiliwa kwani wanatamani kuwaona nyota wao wakijiandaa,”.

“Tumefika hapa pamoja na timu ilipokuwa ikiwasiri kutoka kambini lakini mara baada ya kuingia sisi tumezuiliwa sijapendezwa kwani nilitaka kuwaona leo kabla ya mchezo,” anasema.

Advertisement