Muntari tena? Songo nje miezi miwili

Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea Machi 6 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, ambako Songo aliumia wakati anajaribu kuuwahi kwa kuupiga kichwa mpira, ndipo kipa Muntari ambaye alikuwa langoni akagongana naye na inaelezwa alipoteza fahamu.
BAADA ya tukio la mshambuliaji wa JKT Tanzania, Edward Songo kugongwa na kipa wa Mashujaa, Patrick Muntari na kuwahishwa Hospitali ya Muhimbili, sasa atatakiwa kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili.
Tukio hilo lilitokea Machi 6 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, ambako Songo aliumia wakati anajaribu kuuwahi kwa kuupiga kichwa mpira, ndipo kipa Muntari ambaye alikuwa langoni akagongana naye na inaelezwa alipoteza fahamu.
Gari la polisi pamoja na lile la wagonjwa yaliingia uwanjani na kumchukua Songo na kuondoka kwa kasi na kupelekwa uwanja wa ndege ambako aliwahishwa Hopitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Taarifa kutoka kwa chanzo cha ndani zilisema kuwa mchezaji huyo aliumia kichwani, lakini pia meno yake yalihama kutoka kwenye sehemu yake ya asili.

Mwanaspoti jana lilimtafuta Songo ili kufahamu hali yake ambapo alisema anaendelea vizuri, lakini madaktari wamemweleza kuwa anatakiwa kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili.
“Namshukuru Mungu sana kwa uponyaji wake, nakumbuka niligongana na mtu uwanjani, baada ya hapo sikujua kilichoendelea.
“Lakini kwa sasa nimetoka hospitalini naendelea vizuri, ila daktari ameniambia natakiwa kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili, baada ya hapo nitajua ni kitu gani kitafuata.”
Oktoba 28,2012, Muntari akiwa na JKT Tanzania, alimuumiza Nsa Job kipindi hicho akiwa mshambuliaji wa Coastal Union, ambaye naye aliwahishwa Muhimbili kwa matibabu, mchezo huo ulichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na jeraha hilo likamfanya Job aachane na soka. Job sasa anaishi Hong Kong.