Msimu wa 2020/21 jinsi unavyoipa nafasi Yanga kutwaa Ubingwa

Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/2021 imeingia raundi ya pili huku Yanga ikionekana iko moto kwani inaongoza ligi huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote hadi sasa.
Yanga ambayo ilianza ligi kwa kusuasua imeonekana iko moto hivi sasa na kuwapa presha kubwa watani zao wa jadi Simba ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo.
Kitendo cha Simba kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo ndio kimeapa hasira Yanga ambayo msimu huu ilisajili karibu kikosi kizima na lengo ni kuhakikisha inarudisha heshima yao.
Simba haikufanya usajili mkubwa sana msimu huu kutokana na kuwa na imani kubwa na kikosi chao msimu huu ni kama ilivyo kwa Azam ambayo nayo msimu huu haikuongeza wachezaji wengi
Hadi sasa usajili upi umeonekana kulipa?
Kwa uande wa Yanga licha ya kwamba ilianza ligi kwa kusuasua huku ikibezwa kwa kucheza soka lisilovutia lakini kwa siku za karibuni imeonekana kutulia na kucheza soka la maelewano makubwa na kama ikiendelea hivyo basi ubingwa msimu huu utatua Jangwani.

Ilisajili wachezaji 12 mwanzo wa msimu ambapo nane waliingia moja kwa moja kikosi cha kwanza na baadhi wanafanya vizuri wakati wanne wanaanzia benchi.
Wachezaji ambao waliingia moja kwa moja kikosi cha kwanza ni beki, Bakari Mwamnyeto aliyetokea Coastal Union, Kibwana Shomari (Mtibwa Sugar), Yassin Mustapha (Polisi Tanzania),Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda kutoka AS Vita ya Congo, Michael Sarpong (Rayon Sport Rwanda), Carlos Carinhos (Angola) na Farid Mussa aliyetokea klabu ya Tenerife ya Hispania wakati wanaoanzia benchi ni Yacouba Sogne (Ghana), Zawadi Mauya (Kagera Sugar), Wazir Junior (Mbao FC) na Abdallah Shaibu Ninja.
Mwamnyeto ambaye ni nadra kumkuta nje ya kikosi cha kwanza ametengeneza pacha nzuri na mghana, Lamine Moro na hivyo Yanga kuwa na ukuta mgumu usiopitika kirahisi na ndio maana timu hiyo imeruhusu mabao machache kwenye ligi.
Mabeki hao wanashirikiana na Yassin na Kibwana ambaye ameonekana kuziba vema pengo la Juma Abdul ambaye aliachwa mwisho wa msimu uliopita na sasa anacheza soka la kulipwa Zambia.
Kwa upande wa Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda wameonekana kuimarisha Yanga katikati ya uwanja na pembeni.
Tuisila ni winga mwenye kasi ambaye amekuwa akiwalaza na viatu mabeki wa timu pinzani na mbio zake zimekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo wakati Mukoko ameituliza timu katikati akilinda vema ukuta wa timu yake usipate madhara huku pia akifunga mabao kwani mpaka sasa ana mabao mawili.
Kwa upande wa Carlinhos mwenye mabao mawili kwenye ligi ni mchezaji kipenzi cha mashabiki wa Yanga na ndio maana hata mapokezi yake yalitia fora lakini bado hajaweza kuonyesha ubora uliotarajiwa na wengi huku hivi sasa akiwa hachezi mara kwa mara bila kujulikana nini tatizo vivyo hivyo kwa Farid ambaye ameshindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa na mashabiki na kuonekana kama ni usajili uliofeli licha ya kuwa na pasi tatu za mabao mpaka sasa huku akiwa hajafunga bao.
Wachezaji wengine ambao usajili wao umeonekana hauna maajabu ni Wazir Junior ambaye hana namba kikosi cha kwanza na ana bao moja tu kwenye ligi, Zawadi Mauya na Abdallah Shaibu Ninja.
Pia Yanga imefanya usajili wa kumuongeza mshambuliaji, Said Ntibanzokiza’Saido’ wa Burundi kwenye dirisha dogo la usajili ambaye ameonekana ni moto wa kuotea mbali kwani mpaka sasa ana bao moja kwenye ligi huku akiwa na pasi tatu za mabao lakini pia alifunga mabao mawili katika mchezo wa kirafiki ambao ulikuwa wa kwanza kwake akiwa ndani ya jezi ya Yanga.
Wote Wanafunga
Unaweza usiamini lakini ni Yanga sasa inabebwa na wachezaji wote katika kikosi hicho na haitegemei washambuliaji pekee kufunga bali hata mabeki nao wamo katika kutupia jambo ambalo limekuwa likiibeba sana timu hiyo na kuvuna pointi katika michezo mingi.

Wachezaji Sarpong, Lamine, Yacouba na Deus Kaseke wote wana mabao manne kila mmoja, wakati Carlinhos, Mukoko,Tuisila wakiwa na mabao mawili kila mmoja huku waliofunga bao moja wakiwa ni Waziri Junior, Saido na Haruna Niyonzima.
Ujio wa Kaze
Ujio wa kocha Cedrick Kaze ndani ya kikosi cha Yanga umeongeza kitu ndani ya timu hiyo kwani kcoha huyo ameonekana ana mbinu nzuri za kiufundi na anajua kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia hivyo kuwa na morali kubwa uwanjani.
Tangu atue Oktoba 15 na kuanza kuinoa timu hiyo ameiongoza katika michezo 12, akishinda tisa na kutoka sare michezo mitatu.
Simba
Wekundu wa Msimbazi ambao ndio mabingwa watetezi msimu huu wameonekana wamekaliwa kooni na watani zao wa jadi Yanga hiyo kama wasipochanga karata zao vizuri kwenye mzunguko wa pili basi watautema ubingwa mapema msimu huu.
Msimu huu walisajiliwa wachezaji sita tu ambao ni Joash Onyango, Rally Bwalya, Chriss Mugalu, David Kameta (Duchu), NA Ibrahim Ame.
Kati ya wachezaji hao ni Onyango tu ambaye amepata nafasi ya moja kwa moja kikosi cha kwanza licha ya kwamba mashabiki wa klabu hiyo wameonkana wako nusu nusu katika kukubali uwezo wake lakini wachezaji wengine waliobaki bado hawajaonyesha maajabu ya kusajiliwa na klabu hiyo hivyo Simba kubebwa zaidi na wachezaji waliokuwepo tangu msimu uliopita.

Onyango anacheza na Pascal Wawa lakini pacha yao licha ya kuruhusu mabao matano imeendelea kunyooshewa kidole kuwa inayumba na ikipata washambuliaji wenye kasi basi mambo yanaweza kuwa magumu kwao kwani mabeki wote hao wawili ni wazito hivyo taarifa zilizopo ni kwamba uongozi wa klabu hiyo umeingia chimbo kusaka beki wa kuwaongezea nguvu.
Mugalu mwenye mabao matatu kwenye ligi alionekana kuanza kuja vizuri na kuwateka mashabiki wa klabu hiyo lakini majeruhi yakamrudisha hatu nyingi nyuma wakati Rally amekuwa hapati nafais ya kuanza kikosi cha kwanza kama ilivyo kwa Morrison, Duchu na Ame.
Simba inabebwa zaidi na John Bocco mwenye mabao nane akisaidiwa na Clatous Chama aliye na mabao sita na pasi sita za mabao, Meddie Kagere mwenye mabao matano pamoja na Konde Boy, Luis Miquissone mwenye bao moja lakini akitoa pasi saba za mabao.
Wachezaji hao watatu watakuwa wamewekwa katika maombi na mashabiki wa Simba ili wasikumbwe na majeruhi kwani kama wawili tu wakipata tatizo basi timu hiyo inaweza kuwa katika wakati mgumu maana inaathiriwa zaidi na kutegemea baadhi ya wachezaji.
Azam
Azam ilianza kwa kasi msimu huu na kuongoza ligi kwa wiki kadhaa lakini ghafla mambo yamegeuka na sasa iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.
Ilisajili wachezaji saba tu mwanzo wa msimu ambao ni Prince Dube(Highlanders Fc Zimbabwe), Ally Niyonzima (Rayon Sports Rwanda), Ayoub Lyanga (Coastal Union), David Mapigano Kisu ( Gor Mahia Kenya), Awesu Awesu (Kagera Sugar), Ismail Aziz Kada (Prisons) na Emmanuel Charles kutoka Mbao.
Kati ya wachezaji wote hao ni Dube pekee aliyeipa matunda Azam mpaka sasa kwani ameifungia mabao sita kwenye ligi huku akitoa pasi tano za mabao pamoja na kipa David Kissu ambaye amedaka mechi 14 za mzunguko wa kwanza kati ya 16.

Hata hivyo Azam imepata pengo baada ya Dube kuvunjika mfupa wa mbele wa mkono wa kushoto uitwao Ulnar na hivyo kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi na anaweza kukaa nje ya uwanja kwa wiki nne au zaidi.
Kwa upande wa kipa Kissu alianza vizuri lakini kitendo cha kuruhusu mabao mepesi kilisababisha kuwekwa benchi katika michezo miwili dhidi ya Gwambina na Namungo hivyo mwenzake, Bendictor Haule kuchikua namba lakini nae akazingua hivyo Kisu kurejea tena golini katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Kufanya vibaya katika mechi sita mfululizo zilizopita ni kama kumeipunguza kasi timu hiyo na kuindoa taratibu katika mbio za ubingwa hivyo ili irejee katika vita hiyo inabidi ipambane hasa huku ikipiga maombi Yanga na Simba zipoteze baadhi ya mechi zake kwenye mzunguko wa pili.
Ilianza kuchapwa na KMC na Yanga bao 1-0, kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na Biashara United, ikatoka suluhu na Gwambina FC, ikatoka sare ya mabao 2-2 na Namungo na Ruvu Shooting.
Msikie Kiemba
Kiungo wa zamabi wa Yanga na Simba, Amri Kiemba alisema Yanga msimu huu wamejua kuwatengeneza wachezaji wao kiakili na kuwa na roho ya upambanaji inayowasaidia kupata matokeo mazuri.
“Yanga imesajili wachezaji wenye kiwango msimu na wanajitolea kwa asilimia 100 na hiyo inatokana na wenyewe kuwajenga wachezaji wao kisaikolojia hivyo kama wataendelea hivyo wana asilimia kubwa za kutwaa ubingwa,“ anasema kiemba.
Anaongeza “pia hata Simba bado wana wachezaji wenye uwezo mkubwa muhimu ni kujiongeza na kucheza katika ubora wao kwani vita ya ubingwa msimu huu ni kubwa.
“Azam walianza vizuri ligi lakini baadae kawashuka hivyo tatizo nililoliona hivi sasa kwao ni wamepoteza morali ya kupambana uwanjani hivyo kocha wao anatakiwa kulifanyia kazi hilo ili warejee katika mbio za ubingwa kwani bao wana wachezaji wazuri wa kupambania ubingwa,” anasema Kiemba.