Msimu mpya BDL/WBDL, kazi imeanza DonBosco

Muktasari:
- Kamishina wa ufundi na mashindano hayo, Haleluya Kavalambi alisema ligi ya mwaka huu itachezwa katika mzunguko mmoja, baada ya hapo timu nane za juu zitacheza hatua ya robo fainali.
LIGI ya kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), inatarajia kuanza kesho kwa michezo miwili kupigwa katika Uwanja wa Donbosco Upanga na utaishuhudia UDSM Outsiders itakipiga dhidi ya JKT, huku ikitanguliwa na DB Lioness ikikwaruzana dhidi ya mpinzani wake mkubwa Vijana Queens ikiwa ni michezo ya ufunguzi kwa wanaume na wanawake.
Kamishina wa ufundi na mashindano hayo, Haleluya Kavalambi alisema ligi ya mwaka huu itachezwa katika mzunguko mmoja, baada ya hapo timu nane za juu zitacheza hatua ya robo fainali.
Ligi hiyo ambayo ndiyo maarufu zaidi katika mchezo huo nchini, inashirikisha timu 16 za wanaume na 16 za wanawake na mshindi inapata pointi tatu na iliyofungwa moja.
Alisema robo fainali itachezwa kwa kila timu kucheza mara tatu ‘best of three play off’ na mshindi wa kwanza atacheza na wa nane, wa pili na wa saba, wa tatu na wa sita na wa nne na wa tano na nne zilizoingia nusu fainali, zitacheza kwa kucheza mara tano ‘best of five play off’, huku zitakazoshika nafasi tatu za mwisho zitashuka daraja.

UDSM na JKT zinakutana kwa mara ya pili na mara ya mwisho zilikutana katika fainali ya BDL mwaka jana, katika fainali hiyo JKT ilishinda katika michezo 3-1 na mchezo wao unasubiriwa kwa hamu.
Hata hivyo, UDSM itawakosa nyota wao, Mwalimu Heri, Evance Davies, Tryone Edward waliotimukia Stein Warriors, Baraka Sabibi, Jimmy Brown waliojiunga na JKT.
Kocha wa UDSM, Mohamed Mgweno alisema licha wachezaji hao kuondoka nafasi zao zimezibwa na waliosajiliwa kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza.
JKT inajivunia nyota wapya kama Jordan Manang aliyetokea Mchenga Star, Baraka Sabibi, Jimmy Brown (UDSM Outsiders), Alfan Mustafa (Vijana ‘City Bulls’) na Adam Lutungo (Mgulani JKT).
Baada ya michezo hiyo, siku ya pili zitapigwa mechi nyingine kwa mujibu wa ratiba, Kigamboni Queens itaikaribisha UDSM Queens, huku kwa upande wa wanaume, Kurasini Heat itacheza dhidi ya Mgulani JKT na Twalipo Queens dhidi ya City Queens.

KURASINI WAPANIA
Naodha wa Kurasini Heat, Dominick Zacharia alisema wamejipanga vizuri kushinda dhidi ya Mgulani JKT na licha ya ukosefu wa pesa za maandalizi, wachezaji wenzake wameahidi kupambana kushinda mchezo huo.
“Tumepambana sana kutafuta fedha na kampuni tulizoziendea walitujibu na kutoa ahadi tu,” alisema Zacharia na kuongeza wadau wachache walioko Kurasini wanajitolea.
“Michango imekuwa ikitolewa na mdau mmoja mmoja, kwa kweli sina budi kuwashukuru,” alisema Zacharia.
Aliwapongeza wachezaji wake kwa uvumilivu wanaofanya wa kuipambania timu yao huku wakijua timu haina fedha.
Kurasini iliwahi kuwa bingwa wa ligi hiyo mwaka 2020 na 2021 ilishuka daraja baada ya kuondokewa na nyota wake wote.

Tausi Royals yashusha tisa WBDL
Kiongozi wa timu hiyo, Gerald Gulaka ametangaza majina ya nyota wao tisa ambao anadai usajili huo umetokana na malengo waliyojiwekea.
Alisema Tausi imesajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuimarisha kikosi chao katika ligi ya mwaka huu ambao ni Tumaini Ndossi aliyetokea Vijana Queens, Rehema Joseph (JKT Stars), Mahewa Allan (DB Lioness) na Tumwagile Joshua (DB Troncatti).
Wengine ni Happya Danford (Vijana Queens), Ramla Mohamed (Mchenga Queens), Kelta Mwenda (JKT Stars), Jesca Mbowe (Pazi Queens) na Lucy Masele (UDSM Queens).
“Tunaamini nyota hawa watakuwa na msaada mkubwa sana kuisaidia timu kufikia malengo ya mwaka huu,” alisema Gulaka.

Akizungumzia kuhusu ligi ya mwaka jana, alisema ilifanya vizuri kutokana na msimu huo kuwa ni wa kwanza kwao na ilishinda michezo 25, kati ya michezo 30 na kucheza robo fainali.
“Haya ni mafanikio makubwa kabisa kwa timu ambayo ndiyo ilikuwa inacheza ligi kwa mara ya kwanza,” alisema Gulaka.