Msimbazi kama kawa, kama dawa

Muktasari:
Bao la dakika ya 87 lililofungwa na mtokea benchi, Awadh Juma ‘Maniche’ lilitosha kuipa Simba ushindi wake wa 9 kati ya mechi 10 za Ligi Kuu ikiwa chini ya kocha Mganda Jackson Mayanja aliyeiongoza timu hiyo katika jumla ya mechi 12 tangu Januari 12, 2016.
WAMEBANA mwisho wameachia. Wekundu wa Msimbazi, Simba jana Jumapili waliendeleza wimbi la ushindi Ligi Kuu Bara kwa kuifunga Prisons ya Mbeya bao 1-0 katika mchezo mkali ambao maafande hao walikaza mwanzo mwisho.
Bao la dakika ya 87 lililofungwa na mtokea benchi, Awadh Juma ‘Maniche’ lilitosha kuipa Simba ushindi wake wa 9 kati ya mechi 10 za Ligi Kuu ikiwa chini ya kocha Mganda Jackson Mayanja aliyeiongoza timu hiyo katika jumla ya mechi 12 tangu Januari 12, 2016.
Maniche alifunga bao hilo baada ya kupewa krosi tamu na Jonas Mkude na kuukokota mpira akipunguza mabeki wa Prisons kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Beno Kakolanya.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 54, nne zaidi ya ilizonazo watetezi wa ligi hiyo, Yanga na saba zaidi na ilizonazo Azam ambao wikiendi wote walikuwa kwenye majukumu ya kimataifa za Afrika.
Hata hivyo Simba imecheza mechi 23 wakati Yanga imecheza 21 na Azam imeshuka uwanjani mara 20 tu na zote ziliwasili jana kutoka Afrika Kusini na Rwanda.
Katika mchezo huo uliochezeshwa vema na mwamuzi, Jacob Adongo kutoka Mara, Prisons walionekana kuikamia Simba na kuibana mwanzo mwisho, huku ikifanya mashambulizi yake kwa kushtukiza karibu muda wote wa mchezo huo.
Mabadiliko ya kipindi cha pili yaliyofanywa na Mayanja yaliisaidia Simba kuikimbiza Prisons na kujipatia bao hilo pekee dakika tatu kabla ya kumalizika mchezo na kuzidi kuwapa raha mashabiki wa Msimbazi.
Simba: Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, Justice Majabvi/ Awadh Juma, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamis Kiiza/Paul Kiongera, Ibrahim Ajib na Mussa Hassan Mgosi/Danny Lyanga.
Prisons: Beno Kakolanya, Salum Kimenya, James Mwasote, Lugano Mwangama, Laurian Mpalile, Jumanne Elfadhil, Lambert Sabiyanka, Juma Seif/ Fred Chudu, Mohammed Mkopi, Jeremiah Juma/Meshack Seleman na Benjamin Asukile.
Katika mechi nyingine za ligi zilizochezwa jana, Mgambo JKT ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya 1-1 na Mwadui FC, iliyotangulia kupata bao kupitia Morris Kaniki kabla ya Fully Maganga kusawazisha. Mjini Shinyanga Kagera Sugar iliifumua Coastal Union kwa mabao 4-0 wakati Majimaji ikitamba nyumbani kwa kuilaza Stand United bao 1-0 lililofungwa na Peter Mapunda.
Ligi hiyo itaendelea tena leo Jumatatu kwa mchezo mmoja kati ya African Sports dhidi ya Mbeya City.