Mpepo matumaini kibao Zambia

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Eliuter Mpepo ambaye amejiunga na Tridents FC amejawa na matumaini ya kufanya makubwa akiwa na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Zambia kama ilivyokuwa wakati akiwa na Buildcon F.C.

Kwa mara nyingine tena, Mpepo amerejea Zambia kucheza soka la kulipwa baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Tridents FC akitokea Mtibwa Sugar.

Akiongea na gazeti hili baada ya kutua Zambia, Mpepo alisema, ”Nimepokea meseji nyingi zikinitakia kheri, asanteni nyote, nimeamua kurudi Zambia kwa sababu ni nchi nzuri ambayo nimewahi kuishi miaka michache iliyopita,”

Mpepo anakumbuka namna ambavyo maisha yake Zambia yalikuwa wakati akiichezea Buildcon F.C. kwa kusema, “Wazambia ni watu wenye upendo, nilifurahia maisha huku na nakumbuka kila ambacho nilihitaji kama mchezaji nilipewa, naamini nitakuwa msaada kwa timu yangu ya sasa na kuifanya kufikia malengo.”

Ndani ya msimu wake wa kwanza Mpepo aliifungia Buildcon F.C. mabao 10 kabla ya kwenda Msumbiji kuichezea CD Costa do Sol.