Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gomes amtega Mkude Simba

KIKOSI cha Simba jioni ya leo kitashuka Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kula kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Didier Gomes akimruhusu kiungo mkabaji wake, Jonas Mkude kuanza tizi na wenzake kwa masharti maalumu.

Mkude alikuwa amesimamishwa kwa muda wa kama mwezi mmoja uliopita kwa utovu wa nidhamu, lakini Kamati ya Nidhamu iliamua kumpiga faini ya Sh2 milioni na kumfungulia, na kocha Gomes naye amemruhusu kujiunga mazoezini, lakini baada ya kikao kizito na nyota wenzake, kisha akatoa masharti kwa kiungo huyo na mwingine kuwa wakijichanganya wajue inakula kwao mazima.

Mchana wa Jumanne kabla ya kwenda mazoezini kulikuwa na kikao kizito kati ya Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez, benchi la ufundi lililoongozwa na Gomes na wachezaji kujadili kurejea tena kikosini Mkude.

Katika kikao hicho wachezaji walionekana kuleta ugumu kwa madai ya kutaka zipite kwanza mechi 10 ndipo Mkude ajiunge na wenzake katika mazoezi na ratiba nyingine za timu ambazo zinaendelea kila siku.

Baada ya mvutano na majadiliano ya huku na kule, Gomes aliwaambia wachezaji kuwa tukio la Mkude lilitokea wakati timu haipo chini yake, hivyo wachezaji wanatakiwa kusahau ya nyuma na kumsamehe mwenzao arudi kambini.

Gomes baada ya kauli hiyo aliwaeleza wachezaji kuanza upya na atakuwa muumini wa kusimamia nidhamu kwenye maeneo yote na kama akitokea mmojawapo amekwenda tofauti bila ya sababu atakutana na adhabu.

Baada ya kutoa kauli hiyo, nahodha wa Simba, John Bocco akiwakilisha wachezaji wenzake alieleza wamemsamehe Mkude arudi kambini kuendelea na majukumu kama awali.

Mkude aliingia kambini na jioni alikwenda katika uwanja wa mazoezi ila kwa kuwa hakuwepo katika timu kwa muda mrefu hakufanya mazoezi na wenzake alifanya binafsi pembeni pamoja na beki Erasto Nyoni.

Hata hivyo, Gomes alisema Mkude ni mchezaji mzuri lakini anatamani kumuona zaidi.

“Ili mchezaji aweze kupata nafasi ya kucheza katika kikosi changu anatakiwa kufanya kazi na kuonyesha ubora katika mazoezi pamoja na michezo na ikiwa tofauti na hivyo itakuwa ngumu kutumika kwani nina kikosi chenye wachezaji wengi bora,” alisema Gomes.

AACHWA DAR NA ONYANGO

Katika hatua nyingine kikosi cha Simba kiliondoka na wachezaji 20 kwenda Dodoma kwa maana hiyo kuna 18, ambao watavaa jezi katika mchezo wa leo na wengine wawili watabaki jukwaani.

Miongoni mwa wachezaji ambao wamebaki ni Mkude, Nyoni, Ally Salim, David Kameta, Joash Onyango, Chriss Mugalu na wengineo ikiwemo wale ambao walisajiliwa kwa ajili ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wachezaji waliobaki Dar hawatakuwa mapumziko, bali jana jioni walikuwa na ratiba binafsi ya kufanya mazoezi mbalimbali ambayo yalisimamiwa na mtaalamu wa tiba za viungo, Mjerumani Paul Gomes ambaye naye hakwenda Dodoma.

Wachezaji walioondoka ni Aishi Manula, Benno Kakolanya, Shomary Kapombe, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Ibrahim Ame, Gadiel Michael, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Rally Bwalya, Mzamiru Yassin, Luis Miquissone, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Clatous Chama, Meddie Kagere, Miraji Athumani, Hassan Dilunga, Taddeo Lwanga, Bernard Morrison na Perfect Chikwende.

Kocha wa Simba, Gomes alisema wanakwenda Dodoma kutafuta pointi tatu jambo ambalo linawezekana kutokana na maandalizi ya mchezo huo yalivyofanyika, lakini kutokana na alivyowafuatilia wapinzani wake.

“Nilitangaza muda wa kuwaangalia, Dodoma ni timu nzuri na tumekuja huku kuwakabili kutokana na ubora wao ili kuwazidi na kupata pointi tatu ambazo ndio malengo yetu makuu,” alisema Gomes.