Prime
Mo, Barker... Kikao kizito Sauzi
WAKATI Simba ikikamilisha usajili wa miaka miwili winga raia wa Afrika Kusini, Keletso Makgalwa, Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amefanya kikao kizito na kocha wa klabu hiyo Steve Barker nchini Afrika Kusini na miongoni mwa vitu vikubwa alivyovizungumzia ni usajili na taswira ya benchi la ufundi kwa msimu ujao.
Simba inadaiwa imekamilisha usajili wa winga machachari Makgalwa, mwenye umri wa miaka 29.
Usajili huo unatajwa kama pigo kubwa kwa watani zao wa jadi, Yanga ambayo ilikuwa kwenye mapambano wa kuwania saini ya mchezaji huyo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, alijaribu kila mbinu kumshawishi Makgalwa ili waungane tena kama walivyofanya walipokuwa katika klabu ya Mamelodi Sundowns, lakini winga huyo ameamua kuchagua kuvaa uzi mwekundu.
Makgalwa amekubali kutua Msimbazi baada ya kuvutiwa na mipango ya Simba kwa msimu ujao.
Katika klabu hiyo ya Msimbazi, winga huyo atafanya kazi chini ya kocha mkuu raia wa Afrika Kusini, Barker.
Makgalwa anajiunga na Simba akitokea klabu ya Sekhukhune United ya nchini kwao, ambako ameacha rekodi nzuri akicheza mechi 66 katika mashindano yote, huku akifunga mabao 6 na kutoa pasi za mabao (assists) 20.
Uhamisho huo umekamilika wakati hivi karibuni Mo Dewji alikuwa nchini Afrika Kusini ambapo alifanya mkutano wa waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya kampuni zake pamoja na uwekezaji wake kwenye kikosi hicho cha Msimbazi kupitia taasisi yake ya Mo Foundation.
Huyu ni mmoja kati ya matajiri wenye mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Simba tangu alipoanza uwekezaji wake miaka kadhaa iliyopita, huku timu hiyo ikifanikiwa kutwaa makombe makubwa yakiwemo ya Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo, kufika robo fainali ya michuano ya Caf zaidi ya mara nne na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Chanzo cha taarifa hiyo kutoka Simba, kilisema Mo Dewji alimpongeza kocha Barker kutokana na kazi nzuri aliyoifanya msimu uliyoisha.
Kocha Barker aliisaidia Simba kunyakua taji la Muungano Aprili 29, ikiifunga Yanga bao 1-0 na Kombe la Shirikisho la CRDB ikishinda bao 1-0 dhidi ya Azam, mechi hiyo ilipigwa Pemba Julai 4, 2026, katika Ligi Kuu ikimaliza nafasi ya pili kwa pointi 73, ikizidiwa na mtani wake Yanga alama mbili.
Chanzo hicho kilisema: “ Walikuwa na kikao kizuri na jambo la kwanza kocha Barker alihitaji kuendelea kufanya kazi na benchi la ufundi alilokuwa nalo msimu uliyopita kama kocha msaidizi Selemani Matola, meneja Patrick Rweyemamu na mratibu wa timu Abbas Ally ambao baadhi mikataba yao ilikuwa inamalizika mwishoni mwa mwezi huu, hivyo aliamuru wapewe mikataba mipya.’’
Kiliongeza :”Mbali na benchi la ufundi pia walijadili usajili wa wachezaji wapya ambapo bosi huyo alimtaka kocha huyo kushirikiana na viongozi waliopo kwenye kikosi hicho kuhakikisha Simba inafanya usajili imara utawapa nafasi ya kuwika kwenye michuano ya kimataifa, pamoja na ligi za ndani.
Chanzo hicho kilisema suala la Matola, ambaye alikuwa akiwaniwa na timu kadhaa zilizopanda daraja ikiwemo timu yake ya zamani ya Geita Gold lipo mezani.