Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mlandege ilivyopiga bao Zanzibar

MLANDEGE Pict

Muktasari:

  • Wababe hao wa mjini Unguja, walitwaa taji hilo dakika za jioni baada ya ligi hiyo kuongozwa kwa muda mrefu na Mwembe Makumbi iliyopanda daraja msimu huu iliyomaliza katika nafasi ya nne nyuma ya Mlandege, KVZ na Mafunzo zilizomaliza juu yake katika msimamo wa mwisho wa ZPL.

MLANDEGE imeandika historia ya kubeba ubingwa wa nane wa Ligi Kuu Zanzibar, baada ya wikiendi iliyopita kumaliza kileleni ikizipiga bao timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo.

Wababe hao wa mjini Unguja, walitwaa taji hilo dakika za jioni baada ya ligi hiyo kuongozwa kwa muda mrefu na Mwembe Makumbi iliyopanda daraja msimu huu iliyomaliza katika nafasi ya nne nyuma ya Mlandege, KVZ na Mafunzo zilizomaliza juu yake katika msimamo wa mwisho wa ZPL.

Mlandege imemaliza msimu ikifikisha pointi 62 sawa na ilizokuwa nazo, KVZ, lakini uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa umeibeba na kuipa taji hilo linalokuwa moja pungufu ya waliyonayo mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, KMKM wenye mataji tisa wakiwa vinara.

Ushindi wa mabao 4-2 mbele ya New City, timu iliyoshuka daraja mapema, uliwapa jeuri wababe hao licha ya KVZ nayo kupata ushindi wa 1-0 mbele ya Kipanga katika mechi za kufungia msimu zilizopigwa kwenye viwanja vya Mao A na Mao B mjini Unguja zote zikicheza kuanzia saa 10:00 jioni.

MLA 01

Mlandege imemaliza na jumla ya mabao 67 ya kufunga na kufungwa 21, ikiwa na maana ina tofauti ya mabao 46, wakati KVZ imefunga 35 na kufungwa 12, hivyo tofauti yake ni mabao 23 yaliyoizuia kuwapiku mabingwa hao waliotoa pia Mfungaji Bora wa msimu huu, Abdallah Idd Pina.

Pina aliyeandika rekodi ya kufunga hat-trick mbili katika mechi moja wakati wanaizamisha Tekeleza FC kwa mabao 11-1, yeye akifunga saba, amemaliza msimu huu akiwa na mabao 21 na asisti 12 akiipiku hadi rekodi ya msimu uliopita iliyowekwa na Seleman Mwalimu ‘Gomes’ aliyekuwa KVZ aliyefunga 20. Gomes kwa sasa yupo Wydad Casablanca ya Morocco iliyomnunua hivi karibuni kupitia dirisha dogo la usajili akitokea Fountain Gate alikokuwa akicheza kwa mkopo kutoka Singida Black Stars.

Katika mechi hiyo ya kufungia msimu, Pina alifunga mabao mawili kati ya manne yaliyosindikiza New City kwenda Ligi Daraja la Kwanza ikishuka daraja sambamba na Mwenge pamoja na Tekeleza, Inter Zanzibar zilizopanda na kushuka msimu huu, Tekeleza na Inter zilipanda msimu huu pamoja na Mwembe Makumbi na Junguni United iliyojiokoa katika dakika za lala salama kurudi ilikotoka.

Mabao mengine ya Mlandege inayoshikilia pia ubingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa misimu miwili mfululizo yaliwekwa kimiani na Said Matola.

MLA 02

Pina alimpiga bao nyota wa KVZ, Michael Joseph aliyekuwa akichuana naye vikali katika mbio za kuwania tuzo ya Mfungaji Bora aliyemaliza na mabao 17 katika nafasi ya pili.

Katika mchezo wa wikiendi, Pina ndiye aliyekuwa Nyota wa Mchezo na kubeba zawadi ya Sh100,000, mbali na kumaliza kama kinara wa mabao wa msimu huu, ilhali Hamis Haji Mbarouk wa New City alitajwa kama Mchezaji Bora mwenye nidhamu katika mechi hiyo na kuvuna Sh 100,000.

MLA 03

TAJI LA NANE

Mlandege imetwaa taji hilo linalokuwa la nane baada ya kupita miaka mitano tangu ilipobeba msimu wa 2019-20, kwani awali ilishabeba mara nne mfululizo katika mwaka 1996, 1997, 1998 na 1999, kisha ikabeba tena mara mbili mfululizo 2001 na 2002 na msimu huu wa 2024-2025.

Katika mechi 30 ilizocheza Mlandege msimu huu ilishinda 18 ikatoka sare nane na kupoteza nne tu, huku KVZ iliyokuwa ikichuana nayo ikishinda mechi 17, ikitoksa sare 11 na kupiteza mbili, ikiwa ndio iliyoruhusu mabao machache zaidi kuliko zote yaani 12 tu ikiwapiga bao hadi mabingwa ambao waliruhusu mabao 21 kama Mafunzo iliyokamata nafasi ya tatu katika msimamo ikivuna pointi  55 kupitia mechi 30.

Kubeba ubingwa huo kumeifanya Mlandge kuwa timu ya kwanza ya Zanzibar kukata tiketi ya ushiriki wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, ikiwa sambamba na Simba na Yanga kwa timu za Tanzania Bara, huku mwakilishi wa Kombe la Shirikisho anasubiri mechi za robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ZFF Cup), ili kuungana na Azam na Singida Black Stars zilizopenya Bara.

Pia imewapa nafasi ya kuzoa kitita cha Sh 50 Milioni za ubingwa sambamba na kombe walikokabidhiwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulidi Mwita aliyekuwa mgeni rasmi wa mechi hiyo ya ubingwa, wakati KVZ ikipata Sh20 milioni za ushindi wa pili, Mafunzo iliyokuwa ya tatu imekomba Sh10 milioni na Mwembe Makumbi iliyomaliza ya nne ikizoa Sh5 milioni.

MLA 05

MAKUMBI ILITIKISA

Licha ya kushindwa kushikilia bomba na kuiachia Mlandege kutwaa taji, Mwembe Makumbi ilionyesha haikupanda daraja kwa bahati mbaya kutokana na ushindani mkali iliyoonyesha katika msimu wa kwanza wa kuicheza ligi hiyo.

Wakali hao waliongoza msimamo wa ligi kwa miezi minne kabla ya kutepeta mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Muungano ambalo lilitwaliwa na Yanga iliyowafunga JKU, waliokuwa watetezi wa ZPL na kudondosha pointi taratibu hadi kuishia ya nne.

Hata hivyo, kuingia katika Nne Bora kumeiweka timu hiyo katika nafasi nzuri ya kushiriki Kombe la Mapinduzi 2026 na Kombe la Muungano kadhalika, lakini ikiwapa furaha mashabiki kwa soka ililokuwa ikilipiga kulinganisha na timu nyingine tatu ilizopanda nazo daraja msimu huu, mbali na kuvuna Sh 5 milioni.

MLA 06

NNE MPYA HIZI HAPA

Timu zilizopanda daraja ni New King inayocheza kwa mara ya kwanza ligi hiyo sambamba na New Stone Town na Fufuni zinazotokea Pemba, huku Polisi ikirejea katika ligi hiyo baada ya kushuka misimu miwili iliyopita.

Tekeleza imeandika rekodi mbaya kwa kucheza mechi 30 bila kuonja ushindi wowote zaidi ya kuambulia sare tano na kupoteza 25.