Beki Mghana anukia Tabora United

Muktasari:
- Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, zimeliambia beki huyo aliyezaliwa Septemba 4, 1999, ni miongoni mwa pendekezo la benchi la ufundi la kikosi hicho chini ya kocha mkuu raia wa Zambia, Simonda Kaunda.
KLABU ya Tabora United, iko katika mazungumzo na beki wa kushoto wa Bibiani Gold Stars, William Ntori Dankyi baada ya kuvutiwa na uwezo mkubwa wa nyota huyo raia wa Ghana aliouonyesha msimu ulioisha wa 2024-25, akikichezea kikosi hicho.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, zimeliambia beki huyo aliyezaliwa Septemba 4, 1999, ni miongoni mwa pendekezo la benchi la ufundi la kikosi hicho chini ya kocha mkuu raia wa Zambia, Simonda Kaunda.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Mkenya Charles Obiny alisema wanaendelea na taratibu za kuboresha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, japo hawezi kueleza ni mchezaji gani wanayemuhitaji hadi watakapomsajili.
Licha ya kauli hiyo, Mwanaspoti linatambua mazungumzo kati ya uongozi wa Tabora na mchezaji huyo yanaendelea vizuri, huku kinachosubiriwa tu ni kukubaliana maslahi binafsi ili atue nchini kwa lengo la kukitumikia kikosi hicho msimu ujao.
Awali, mabosi wa Tabora walikuwa pia katika mazungumzo na kipa raia wa Ghana, Fredrick Asare anayeichezea Asante Kotoko, ingawa dili hilo linaweza kukwama, baada ya uongozi kushindwa kumtumia kwa wakati tiketi ya ndege ya kuja Tanzania.
Baada ya uongozi kushindwa kumtumia tiketi kwa wakati, inaelezwa kipa huyo amesitisha mazungumzo hayo ya kuja Tanzania, huku ikielezwa anakaribia kujiunga na Durban City ya Afrika Kusini, iliyokubali kumlipia mahitaji yote aliyoyahitaji.
Bosi mmoja wa Tabora, alisema mkataba walioingia na moja ya kampuni kutoka Nigeria hivi karibuni wenye thamani ya zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa mwaka, utakuwa ni chachu ya kutimiza masuala yao yote yanayohusu usajili kwa ajili ya msimu ujao.
Fedha hizo ndizo ambazo zinawafanya mabosi wa Tabora kuanza kumpigia hesabu, Dankyi aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo, King Faisal, Hearts of Oak, Tema Youth, Liberty Professionals na Charity Stars zote za kwao Ghana.
Beki huyo msimu wa 2024-25, aliisaidia Bibiani Gold Stars kuchukua ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu.