Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkali wa asisti Simba amfurahisha Fadlu Davids

Muktasari:

  • Ahoua alibainika kupata majeraha madogo ya misuli mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate na alifunga bao moja wakati Simba ikishinda 4-0 na kuanzishiwa programu maalumu na kocha wa viungo, Riedoh Berdien na kumfanya akose mechi ya kirafiki ya sare 1-1 kati ya timu hiyo na Al Hilal ya Sudan.

KIUNGO mshambuliaji wa Simba anayeongoza kwa asisti kwa sasa katika Ligi Kuu Bara, Jean Charles Ahoua amerejea tena uwanjani akiwa fiti kwa asilimia 100 tayari kuivaa Al Ahli Tripoli ya Libya baada ya kuwa nje kwa majerahana kumpa kicheko Kocha Fadlu Davids aliyemtetea pia straika mpya, Lionel Ateba.

Ahoua alibainika kupata majeraha madogo ya misuli mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate na alifunga bao moja wakati Simba ikishinda 4-0 na kuanzishiwa programu maalumu na kocha wa viungo, Riedoh Berdien na kumfanya akose mechi ya kirafiki ya sare 1-1 kati ya timu hiyo na Al Hilal ya Sudan.

Nyota huyo mpya aliyesajiliwa msimu huu kutoka Ivory Coast, alicheza mechi ya pili ya kirafiki ya Simba inayojiandaa kuvaana na Walibya katika Kombe la Shirikisho Afrika, wakati waalipoifunga JKT Tanzania, huku akifunga pia bao moja katika ushindi wa 2-0.

Nyota huyo alifunga bao hilo katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Mwenge jijini Dar es Salaam na kumfanya Kocha Fadlu kupumua wakati kikosi hicho kikitarajiwa kuondoka nchini keshokutwa kwenda Libya kuvaana na Al Ahli Tripoli itakayochezwa Jumapili ijayo.

Simba itaanzia ugenini katika mchezo huo utakaopigwa Septemba 15 kisha kurudiana jijini Dar es Salaam Septemba 22, huku malengo makubwa ya benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo ni kufanya vizuri kwa ajili ya kutinga hatua ya makundi.

Timu hiyo iliyoanzia raundi ya pili ya mashindano hayo, inakutana na Al Ahli ambayo imefuzu hatua hiyo kwa ushindi mnono wa jumla ya mabao 5-1, dhidi ya Uhamiaji ya Zanzibar baada ya kushinda nyumbani 3-1, kisha kuibuka kidedea ugenini 2-0.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids alisema urejeo wa nyota huyo ni jambo muhimu katika kuongeza nguvu ndani ya timu hiyo, huku akiweka wazi kwa sasa kitu wanachokiombea ni kuona wachezaji wote wako katika hali nzuri ya utimamu wa kimwili.

“Kwa sasa kila kitu kinaenda vizuri japo hatujui wale ambao bado hawajamaliza majukumu yao katika timu zao za taifa, tuko kwenye wakati mzuri kwa sababu michezo hii miwili ya kirafiki imetusaidia kututengenezea balansi tofauti tofauti.”

Ahoua aliyewahi kuzitumikia timu za LYS Sassandra na Sewe Sports kisha kukipiga Stella Club Adjame zote za kwao Ivory Coast na msimu huu kujiunga na Simba, alianza taratibu ndani ya kikosi hicho ingawa kwa sasa amekuwa mchezaji tegemeo.

Msimu uliopita akiwa na Stella Club Adjame, nyota huyo alikuwa mchezaji bora (MVP) na alifunga mabao 12 na kuasisti tisa, jambo lililowavutia zaidi mabosi wa Simba kumsajili kutokana na uwezo wake aliouonyesha.

Msimu huu pekee tayari nyota huyo ametwaa tuzo ya Ligi Kuu Bara kwa Agosti, baada ya timu hiyo kupata ushindi katika michezo yote miwili iliyocheza kwa mwezi huo, huku Ahoua akifunga bao moja na kuastisti mara tatu akiwa ndiye kinara wa asisti.


FADLU NA ATEBA

Kocha wa Simba, Fadlu amemkingia kifua mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Lionel Ateba akisema anamwona akifika mbali msimu huu kwa jinsi anavyomsoma mazoezini kambini.

Ateba 25, mwenye uwezo wa kucheza pia winga zote ndiye mchezaji wa mwisho kusajiliwa Simba akitokea USM Alger, alikoondoka akiwa na rekodi ya kucheza mechi 23 katika michuano mbali mbali na kufunga mabao matatu na asisti saba, huku hadi sasa akiwa na kikosi hicho hajaitumikia katika Ligi Kuu, lakini katika mechi ya kirafiki dhidi ya Al Hilal alifunga bao moja.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema, kwa ubora anaomuona nao mshambuliaji huyo na akiunganisha na viungo anaamini kuna kitu kizito kinajengwa msimu hu.

Alisema ni mshambuliaji wa tofauti sana hasa anapokuwa uwanjani unamwona kabisa kuwa ana njaa ya kupata ushindi na ndiyo maana alipopata nafasi aliitumia na kufunga.

“Ni mshambuliaji mzuri, kwani akiwa uwanjani unamuona anavyopambana, wakati bado akiwa mgeni kabisa, hii inaonyesha matumaini makubwa. Ninachotaka ni yeye kujiimarisha na kuungana na wachezaji wenzake hasa viungo ili waweze kuwa na ushirikiano mkubwa wa kutengeneza nafasi na kupata mabao.”

“Namuona Ateba akiwa na msimu mzuri kwa kufunga mabao ya kutosha kwani sasa vimebaki vitu vichache kama kuzoeana na wenzake ili mkali zaidi,” aliongeza Fadlu.