Mirambo: Uganda wameshikilia tiketi yetu ya kwenda Brazil

Muktasari:
Yoyote atakayefungwa katika mchezo wa kesho kati ya Tanzania na Uganda atakuwa ameaga mashindano hayo na kupoteza tiketi ya kwenda Brazil.
Dar es Salaam. Tanzania ‘Serengeti Boy’ inahitaji ushindi tu dhidi ya Uganda kesho Jumatano ili kufufua matumaini yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia Brazil.
Serengeti Boys na Uganda zinaingia katika mchezo huo zikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi zao za kwanza dhidi ya Nigeria na Angola hivyo yoyote atakayefunga katika mchezo huo atakuwa amepoteza tiketi ya kwenda Brazil.
Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema mchezo wao dhidi ya Uganda ndio utawahakikishia kwenda katika fainali za Kombe la Dunia.
"Huu ni mchezo ambao hatuna cha kupoteza zaidi ya ushindi, matokeo mazuri ndio yatatuweka sisi sehemu nzuri ninaimani tutapata pointi tatu muhimu," alisema Mirambo.
Akizungumzia makosa yalijitokeza kwa golikipa wake katika mchezo uliopita, alisema benchi la ufundi limenza kazi ya kuhakikisha kikosi kinakuwa bora kuanzia katika safu ya ulinzi mpaka nyuma hivyo wanafanyia marekebisho madogo madogo kikosi chao.
Kocha mkuu wa Uganda, Samuel Kwasi alisema wanajua mchezo wao utakuwa mgumu, lakini anaamini watapata matokeo yatakayofufua matumaini ya kwenda kombe la dunia.
"Tunajua Tanzania watakuwa wapo 12 uwanjani, lakini hilo halitutishi tunaenda kupambana na tunahitaji matokeoa ya pointi tatu na sio jambo lingine."
Nahodha wa Uganda, Kizito Mugwer alisema anaifahamu Tanzania vizuri baada ya kucheza nao katika hatua ya kufuzu katika fainali hizo hivyo hawawasumbui na lengo ni kuchukua pointi tatu.