Mirambo aachiwe Serengeti Boys

Muktasari:
Wakati tukisubili kuanza kwa mashindano hayo, Serengeti Boys tayari wao wamezidi kujiimarisha kwa kucheza mechi za kirafiki na katika hilo walibeba kombe la COSAFA ambalo walikuwa kama wageni waalikwa.
KOMBE la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa vijana chini ya miaka 17 linatarajiwa kuanza mwakani nchini huku Tanzania ikiwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Wakati tukisubiri kuanza mashindano hayo, Serengeti Boys tayari walianza kujiimarisha kucheza mechi za kirafiki na katika hilo walibeba kombe la COSAFA ambalo walikuwa kama wageni waalikwa.
Lakini kumeibuka sintofahamu baada ya Shirikisho la Soka nchini(TFF) kutaka kuleta kocha mwingine kutoka nje ili kuisongesha timu hiyo katika mashindano ya mwaka huu.
Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mambo yanayoweza kuigharimu timu hiyo iwapo itakuwa mikononi mwa kocha mwingine na kuachana na Oscar Mirambo ambaye ameipigania timu hiyo kwasasa.
PENGO LA MIRAMBO
Vijana hao wamelelewa kwenye mikono ya Mirambo ambaye anafahamu mahitaji yao yote kwani amewakuza kisoka na kuwapa malezi yake kwa asilimia kubwa.
Mirambo ni kocha ambaye alizunguka mikoani kutafuta vijana katika mashindano ya Umitashumta na Umisseta ili kupata wachezaji na leo ndio wanafanya vizuri na kutambua kila tabia ya mchezaji baada ya kukaa na wachezaji hao kambini ambapo kambi yao ilikuwa kwenye hosteli za TTF kwa takribani siku 100 akichuja wachezaji wenye viwango bora zaidi ya wengine.
Kuondoka kwa Mirambo katika benchi la ufundi kunaweza kuleta shida kidogo kwani wachezaji anajua namna ya kuanza na kumaliza nao , labda aletewe mtu ambaye atakubali kufanya kazi na benchi ambalo limepambana na timu hii muda wote.
MFUMO UTATA
Alipoondoka Kim Poulsen wengi walishika vichwa na kusema kwamba hapa soka la vijana limeanza kupotea kwasababu timu hii tangu 2011 mpaka mwaka jana licha ya kwamba aliondoka 2014 na kurejea nchini 2016 ilianza kuonyesha mwelekeo mzuri.
Kim aliwaibua nyota kama Frank Domayo na Mudathir Yahya na wachezaji wengi vijana ambao aliwalea na hakuishia hapo tu kwani soka la vijana linaendeshwa na mfumo wa soka la Danish.
Hata hivyo aliporejea aliweza kuacha mfumo wake na mbinu kwa Oscar Milambo ambaye ameonekana kabisa kwamba ameweza kwa kiasi fulani kufiti viatu vya Kim Poulsen baada ya kukubali kufanya nae kazi kwa ukaribu.
Kim alivyoondoka tena bado tumeona Serengeti Boys wakiendelea kucheza soka safi la utulivu, lakini anapokuja kocha mwingine na kutaka kuanzisha mifumo yake katika kikosi hiki kivyovyote vile ataipotezea radha timu kwani vijana ni ngumu kubadilika haraka kimfumo huku kukiwa na muda mchache.
MORALI YA WACHEZAJI KUSHUKA
Japo sio rasmi sana lakini ilitajwa kwamba wachezaji hawa baada ya kushiriki michuano ya COSAFA walipitia changamoto nyingi lakini hata hivyo benchi la ufundi liliwajenga kisaikolojia na kufanikisha kile ambacho walipanga kukifanya.
Kazi iliyofanya na benchi hilo la kuwajenga wachezaji kisaikolojia kufanya yale yaliyokuwa yametokea ni kama morali kwao na sio kutengwa, badala yake walijituma na mwisho wa siku hata usafiri walioenda nao ulibadilika na kurudishwa kwa ndege.
Hivyo wanajua kabisa kwamba wamepitia mapito magumu na walimu wao, ikifikia hatua kuwabadilishia makocha waliofanya nao kazi vizuri, wanaweza kuharibikiwa kisaikolojia kwasababu wataona kama wazazi wao wanafanyiwa jambo ambalo sio sahihi hata kwao hivyo TFF inabidi wafikilie zaidi kabla hawajafanya maamuzi ya mwisho.
MUDA SIO RAFIKI
Imebakiza miezi mitano tu kabla mashindano hayo kuanza Mei mwaka huu, wakati huo huo Serengeti Boys ikiwa imealikwa kwenda kushiriki mashindano nchini Uturuki ambayo ni moja ya maandalizi kuelekea fainali hizo za Afcon.
Kubadilisha kocha kwa muda fupi uliobaki ni kuwavuruga vijana, ni vyema mabadiliko hayo yangefanywa mapema na kuwaachia klabu ambazo ni kawaida kufanya mabadiliko kadri wanavyoona inafaa maana wachezaji wao wanajitambua na umri wao ni mkubwa kuliko hawa vijana wadogo kabisa.
Mabadiliko hayazuiliki lakini kama kocha analetwa basi aletwe mtu wa kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi akiwa kama mshauri ambaye atawaongozea ushauri akima Mirambo kuhakikisha Serengeti Boys wanafanya vizuri.