Minziro atoa msimamo usajili wa Yondani, Kaseke

Muktasari:
Minziro alikiri kikosi hicho ambacho juzi kilitoka suluhu na JKT Tanzania, licha ya kuanza kuonekana kuimarika, lakini bado kinakosa ushindani kutokana na baadhi ya wachezaji muhimu kuwa majeruhi wa muda mrefu na kushindwa kuisaidia timu.
WAKATI Pamba Jiji ikihusishwa kuwanasa Kelvin Yondani, Deus Kaseke na Habib Kyombo, kocha wa timu hiyo, Fred Felix ‘Minziro’ amefunguka juu ya usajili huo, huku akisisitiza kwamba klabu hiyo haitasajili kwa mihemko bali kuleta mastaa watakaoongeza ushindani ndani ya kikosi hicho.
Minziro alikiri kikosi hicho ambacho juzi kilitoka suluhu na JKT Tanzania, licha ya kuanza kuonekana kuimarika, lakini bado kinakosa ushindani kutokana na baadhi ya wachezaji muhimu kuwa majeruhi wa muda mrefu na kushindwa kuisaidia timu.
Alisema miongoni mwa eneo linalomuumiza kichwa na litakalopewa kipaumbele katika usajili ni ushambuliaji, kwani kwa sasa timu inakosa umakini katika umaliziaji na kushindwa kutumia vyema nafasi nyingi za mabao zinazotengenezwa.
“Tetesi mnazosikia ni watu wameamua tu kujifurahisha, lakini ukweli ni kwamba mchezaji tunayefanya naye mazoezi ndiye tuko tayari kwenda naye vitani huko mbele ya safari dirisha dogo litakapofunguliwa,” alisema Minziro.
“Na wengine ambao unasikia wamesajiliwa tutawaona huko mbele ya safari. hivyo tusubiri tuone Desemba 15 tutajua wachezaji gani tutakaowaongeza lakini tunategemea kuongeza wachezaji watakaoleta ushindani ndani kwenye kikosi chetu,” alisema beki huyo wa zamani wa Polisi Zanzibar na Yanga.
Aliongeza usajili huo wa dirisha dogo utaleta tumaini jipya katika kikosi hicho na hatma yao kwenye Ligi Kuu Bara ili waweze kutoka nafasi za chini na kumaliza katika nafasi za juu na kuepuka kushuka daraja.
“Lazima tuongeze nguvu kwa sababu tumekuwa na mapungufu baadhi ya sehemu kwahiyo watakapokuja wataongeza nguvu zaidi na timu itakuwa na ushindani. Tuna majeruhi wa muda mrefu ambao hatuwezi kuwategemea sana kwahiyo lazima tulete maingizo mapya tulete ushindani,” alisema Minziro.