Minziro akomaa na Mpole, ataja kinachomsumbua

Muktasari:
- Mpole aliyeibuka kinara wa mabao Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/2022 akitupia 17 mbele ya Fiston Mayele wa Yanga aliyefunga 16, ameshindwa kuonyesha makali yaliyozoeleka katika mechi 11 msimu huu akiwa anaitumikia Pamba Jiji ya Mwanza.
KIU ya mashabiki wa Pamba Jiji ni kumuona mshambuliaji, George Mpole akitupia mabao kama walivyomzoea. Kilio hicho kimemfikia Kocha Mkuu Fredy Felix ‘Minziro’ aliyeweka ahadi nzito ya kufufua makali ya nyota huyo huku akitaja kinachomsumbua kwa sasa.
Mpole aliyeibuka kinara wa mabao Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/2022 akitupia 17 mbele ya Fiston Mayele wa Yanga aliyefunga 16, ameshindwa kuonyesha makali yaliyozoeleka katika mechi 11 msimu huu akiwa anaitumikia Pamba Jiji ya Mwanza.
Straika huyo wa zamani wa Geita Gold, alijiunga na Pamba Jiji katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu akitokea FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemkrasi ya Congo hadi sasa amefunga bao moja pekee kwenye ligi huku hatua ya Minziro kuungana na nyota huyo ikiibua matumaini mapya.
Akimzungumzia mchezaji huyo, Minziro aliyekuwa na Mpole ndani ya Geita Gold, aliwaomba mashabiki na wadau kuwa wavumilivu kwani mshambuliaji huyo atarudi kwenye makali kwa sababu wanamfahamu na wanajua namna ya kumsaidia ili awe bora.
“Naamini mpira ni mazoezi hata George Mpole alivyokuwa Geita kuwa mchezaji bora haikuwa rahisi, tulikuwa tunamsukuma sisi mpaka kuja kuchukua ufungaji bora, ni fatiki kama huwezi kuhimili ndiyo mwisho wa siku unaweza kumuona Mpole yuko hivi,” alisema Minziro.
Kocha huyo alisema changamoto ya kupata namba kikosi cha kwanza na kukosa muda wa kutosha wa kucheza katika Ligi ya DR Congo akiwa na FC Lupopo ndizo sababu kiwango chake kimeshuka na hilo linaweza kumtokea mchezaji yeyote.
“Tuendelee kumvumilia, naamini atarudi kwenye ubora wake kama atakubali kutumika jinsi ambavyo tunafanya mazoezi basi naamini atarudi yuleyule kwasababu tumekutana tena mimi na George Wandiba (kocha msaidizi) na yeye Mpole,” alisema Minziro.