Mingange atoa masharti Chama la Wana

Muktasari:
- Mingange aliyeipandisha Mashujaa Ligi Kuu mwaka 2022, akitamba na Azam FC, Ndanda, Lipuli na Tanzania Prisons akiwa na uzoefu wa miaka 37 kwenye ukocha, alitambulishwa Agosti Mosi, mwaka huu huku Kocha Msaidizi akiwa ni Daudi Macha.
BAADA ya kusini mkataba wa mwaka mmoja kufundisha Stand United ya Shinyanga kwa msimu ujao wa Ligi ya Championship, Meja Mstaafu Abdul Mingange amesema uongozi, benchi la ufundi na kamati ya usajili wanapaswa kuzungumza lugha moja katika usajili wa timu hiyo ili kupata kikosi kitakachofanya vizuri.
Mingange aliyeipandisha Mashujaa Ligi Kuu mwaka 2022, akitamba na Azam FC, Ndanda, Lipuli na Tanzania Prisons akiwa na uzoefu wa miaka 37 kwenye ukocha, alitambulishwa Agosti Mosi, mwaka huu huku Kocha Msaidizi akiwa ni Daudi Macha.
Mingange aliliambia Mwanaspoti baada ya kuikubali ofa ya Stand United 'Chama la Wana' aliwapa masharti mawili ambayo ni kuja na benchi lote la ufundi kwa kuleta watu anaoelewana nao na kufanya usajili wa pamoja kati ya benchi la ufundi, kamati ya usajili na uongozi, hakuna mchezaji atakayeletwa bila ridhaa yake.
Alisema baada ya kukamilisha kuunda benchi la ufundi, kwa sasa ameanza usajili kwa kupendekeza majina ya wachezaji anaowafahamu, kuwaita Shinyanga waonwe mazoezini na uongozi huku akiamini usajili makini ndiyo utaisaidia timu hiyo kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
"Cha kwanza ilikuwa kupata benchi la ufundi ambalo tunazungumza lugha moja, hilo nimefanikiwa tumekubaliana. Nashukuru uongozi wa Stand United wakati wameniita kufanya nao mazungumzo tukafikia makubaliano hayo naamini watanisaidia kwenye kazi yangu," alisema Mingange.
"La pili ni kwenye usajili kwa sababu timu ikifeli hapa kupata mafanikio ni ngumu, wachezaji wengi wenye uwezo tunawaita wanakuja wengine wameshacheza daraja la kwanza na Ligi Kuu, nikishamwona naueleza uongozi nawaambia huyu nimemkubali tunajiridhisha kwa kumuangalia mazoezini wakiafikiana tunamsajili."
"Hili jambo la kupandisha timu nina uzoefu nalo cha msingi viongozi waendelee kuniamini kama walivyonipa timu yao, soka siyo mchezo wa matokeo ya siku moja tutakuwa tunacheza na kunaangalia mapungufu kurekebisha ili tufikie mafanikio ya pamoja," alisema Mingange.