Mifumo mitatu kuibeba Simba

Mifumo mitatu kuibeba Simba

WAPINZANI wa Simba Plateau United katika mechi ya mzunguko wa pili Ligi ya Mabingwa Afrika watatua nchini leo saa 7, mchana na Shirika la ndege ya Ethiopia kwa ajili ya mchezo ambao utapigwa kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

Kulingana na Simba walivyocheza pamoja na mbinu ambazo walizitumia katika mechi ya mzunguko wa kwanza na wapinzani wao Plateau United walivyo kuna mifumo mitatu ambayo inaweza kuwabeba na wakaibuka na ushindi katika mechi ya marudiano.

Mfumo wa kwanza ambao Simba wanaweza kunufaika nao ni (4-2-3-1), ambao kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alianza nao katika mechi ya kwanza uliokuwa na mabeki wanne, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein. Pascal Wawa na Joash Onyango, viungo wawili wakabaji walikuwepo Jonas Mkude na Erasto Nyoni.

Katika viungo watatu washambuliaji walianza Hassan Dilunga, Luis Miquissone na Clatous Chama wakati straika alikuwa John Bocco, katika mechi ya kesho mfumo huu unaweza kubadilika kwa kuwepo Bernard Morrison na maeneo mengine yakabaki kama yalivyo.

Faida ya Morrison akipata mpira ni mzuri kukimbia ndani ya boksi akitafuta nafasi ya kufunga mwenyewe, kutengeneza nafasi kwa wenzake kufunga na muda mwingine kuchezewa faulo ambao huwa faida kwa Simba, uwezo wa winga huyo ukikutana na ubora wa Chama, Bocco na Miquisson walioanza katika mechi iliyopita Simba watakuwa bora kwenye kumalizia.

Uwezo wa Morrison na Muquissone katika kimbilia lango la timu pinzani kwenye mfumo huu Simba wanaweza kunufaika na mashambulio ya kushtukiza na wakapata mabao kwa aina hiyo kama ambavyo walifanya katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

Mfumo mwingine ambao unaweza kuibeba Simba (4-3-3), mabeki wanne nyuma wataanza vile vile katika eneo la viungo watatu watakuwepo, Mkude, Nyoni na Chama halafu katika watu watatu wa mbele watakuwepo Miquisson, Bocco na Meddie Kagere ambaye hakucheza kabisa mechi ya kwanza.

Uwepo wa mastraika wawili katika kikosi cha kwanza Simba maana yake mabeki wa timu pinzani hawatakuwa huru kupanda mbele au kucheza kwa kujinafasi, lakini muda wowote wanaweza kufungwa bao aina yoyote ile kutokana na ubora wa Bocco na Kagere katika kufunga nafasi ambazo Chama na Miquissone watatatengeneza.

Mfumo wa tatu ambao Simba huenda wakaanza nao (4-4-2), ambao safu ya ulinzi itabaki vile vile ila katika eneo la kiungo watakuwepo, Mkude, Morrison, Miquissone na Larry Bwalya ambaye anauwezo wa kutengeneza na kupiga pasi za maana kwa washambuliaji wawaili Bocco na Chama.

Simba watanufaika na mfumo huu katika kushambulia kwani watakuwa na zaidi ya wachezaji watano wenye uwezo wa kufunga katika lango la timu pinzani ila shida itakuwa pale ambapo wapinzani wataamua kufanya mashambulizi ya kushtukiza Simba watabaki wachache langoni kwao katika kuokoa.

Katika benchi la wachezaji wa akiba Simba wanaweza kuwepo, Gadiel Michael na Ibrahim Ame ambaye aliingia katika mechi ya kwanza alipotelewa Chama na mabadiliko yake yalikuwa na mlengo wa kwanza kuzuia wengine ambao wanaweza kuwepo, Dilunga, Said Ndemla, Francis Kahata, Ibrahim Ajibu ambao hawa wanauwezo katika kushambulia.

Nahodha wa zamani wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi' alisema kikosi hiko kinawachezaji wengi wazuri ambao wanaweza kufiti katika mifumo yote hiyo mitatu ila kazi itabaki wa kocha, Sven ndio anaweza kuchagua sahihi kati ya hiyo.

"Ambacho nakiona Simba ugenini walicheza kwa kuzuia zaidi ila katika mechi ya nyumbani wanatakiwa kutokupoteza nidhamu ya kuwakaba wapinzani na kufanya mashambulizi mengi ambayo yanatakiwa kutumiwa vizuri kwa kupata mabao kwahiyo mfumo wa kushambulia zaidi ndio unahitajika," alisema Mgosi.

BY THOBIAS SEBASTIAN