Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgosi aipasua Msimbazi

Mussa Hassan Mgosi

Muktasari:

Viongozi wa Simba wamegawanyika juu ya uamuzi wa kumpa mkataba mpya mshambuliaji huyo mkongwe au la.

USAJILI ndani ya klabu ya Simba ni kama umefikia ukingoni kwa baadhi ya nyota wapya na wa zamani kusainishwa mikataba mipya, lakini suala la nahodha wa klabu hiyo, Mussa Hassan Mgosi limekuwa pasua kichwa kwa mabosi wake.

Viongozi wa Simba wamegawanyika juu ya uamuzi wa kumpa mkataba mpya mshambuliaji huyo mkongwe au la.

Habari za ndani ya Simba zinasema suala la Mgosi limeshindwa kujadiliwa katika vikao vyao kwani linasubiri baraka za rais wao, Evans Aveva kuamua.

Chanzo makini ndani ya Kamati ya Usajili Simba, kimesema wao kama kamati hawajagusa kabisa suala hilo ila wanaamini Mgosi ataendelea kuwepo akichukua moja ya nafasi za wachezaji wanaofikiriwa kupelekwa kwa mkopo ambao wanatajwa kuwa ni Hija Ugando na Peter Mwalyanzi.

Habari zaidi zinasema kuwa, uongozi Simba umekubali kununua mkataba wa winga Hassan Kabunda wa Mwadui na jana Jumapili au leo Jumatatu alitarajiwa kusaini mkataba na Wekundu hao.

Chanzo hicho kilisema kuwa wao wamepanga wawe na wachezaji wasiozidi 27 kwani hakuna sababu ya kujaza nafasi zote 30 kama kanuni zinavyotaka. Katika nafasi hizo 27, sita ni kwa nyota wa kigeni na wenye uhakika ni kipa Vincent Angban, beki Mganda, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Laudit Mavugo, Blagnon Goue Frederic na Javier Besala Bokungu ambaye amepewa mkataba wa awali na wanasubiri kumuona kwanza timu ikianza mazoezi kama ataonyesha kiwango.

“Hakuna aliyejadili kuachwa au kumpa mkataba Mgosi, kuna mambo yanayoweza kumfanya asalie kikosini, ila tunasubiri mabosi wetu hasa rais aamue. Watakachosema ndicho kitakachofanywa. Kuna wachezaji wanaofikiriwa kupelekwa kwa mkopo hivyo nafasi ya Mgosi itakuwepo, pia tuna beki mmoja tu wa pembeni Hamad Juma, lazima asajiliwe mwingine.”

Kuhusu beki wa Prisons, Salum Kimenya kiongozi huyo alisema hawakumalizana naye, kauli iliyoungwa mkono na beki huyo aliyethibitishia bado yupo Prisons.

“Nashangaa kuonwa natajwa kusajiliwa Simba wakati hatujamalizana nao, mimi nipo Chuo huku Kiwira, sijawasiliana nao tangu waliposhindwa kufikia makubaliano yetu, nilisema sitaacha ajira kwa Sh 20 milioni yao, mimi ni mchezaji halali wa Prisons,” alisema Kimenya.

Katika orodha mpya ya Simba ambayo Mwanaspoti imepenyezewa wazawa wenye uhakika ni Manyika Peter, Denis Richard, Hamad Juma, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim, Musa Ndusha, Awadh Juma, Novaty Lufungo, Emmanuel Semwanza, Kabunda, Ibrahim Ajib na Danny Lyanga.