Messi, Ronaldo wakabana koo uwanjani

Muktasari:
TOLEO lililopita mwandishi Luca Caioli alizungumzia rekodi za mafanikio ya ufungaji mabao za Ronaldo na Messi kwenye timu zao za Taifa pamoja na mechi ya Argentina na Brazil ambayo ilimkutanisha Messi na rafiki na ‘kiongozi wake’, Ronaldinho. Sasa endelea…
TOLEO lililopita mwandishi Luca Caioli alizungumzia rekodi za mafanikio ya ufungaji mabao za Ronaldo na Messi kwenye timu zao za Taifa pamoja na mechi ya Argentina na Brazil ambayo ilimkutanisha Messi na rafiki na ‘kiongozi wake’, Ronaldinho. Sasa endelea…
Mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Messi alijikuta akimpoza rafiki na kiongozi wake Ronaldinho, alichokifanya Messi ni kuuweka mkono wake mabegani mwa Ronaldinho katika namna ya kumfariji.
Ni picha ambayo ilitoka katika magazeti karibu yote ya siku iliyofuata, picha iliyoonyesha ni namna gani dunia ya soka inaweza kuwa kitu chenye mfano wa ukatili.
Ni Mei 27, 2009, Ronaldo jezi nyeupe, ni jezi au uzi mwingine mkali wa Man United wakati Messi yeye alikuwa amevaa bluu na nyekundu damu ya mzee, jezi ya asili ya Barcelona.
Mmoja alikuwa ndio kwanza ametoka kutangazwa mwanasoka bora ulimwenguni ingawa hakuwa na msimu mzuri wakati mwingine alikuwa ndio kwanza anapaa juu.
Ni mechi iliyotabiriwa kuwa ngumu na katika mazingira sahihi, ni mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyokutanisha timu bora za soka.
Mastaa wawili wanawasili kwenye Uwanja wa Olimpico mjini Roma, Italia wakiwa wamebeba uzito wa mechi hiyo katika mabega yao, macho yote ya mashabiki yalikuwa yakiwatazama wao ingawa wenyewe walionekana kutosumbuliwa na hali hiyo.
Messi ni mchezaji bora lakini habari ya kesho ni kuhusu Man United na Barcelona,’’ alisema Ronaldo siku moja kabla ya mechi hiyo.
Na Messi naye akakubaliana naye pale aliposema kwamba kuwaangalia wachezaji binafsi ni kutoziheshimu timu kubwa, timu mbili ambazo zina wachezaji wengine ambao wanaweza kuwa na umuhimu. Pamoja na kauli hiyo lakini mjadala mkubwa ulikuwa ni Ronaldo dhidi ya Messi au Messi dhidi ya Ronaldo.
Hata kocha wa Man United Sir Alex Ferguson naye aliliangalia jambo hilo ingawa hakuwa tayari kuamua chochote, “Wote ni wachezaji wazuri, wachezaji ambao wanaweza kupika mabao na hata kuyafunga wao wenyewe.
“Pindi wachezaji wazuri wanapofikia kiwango hicho hapo kunakuwa na vitu vingine vidogo vidogo vya ziada, mmoja anaweza kuwa na usiku mzuri au mbaya, zaidi ya hilo nini kingine unachoweza kukisema kwa wachezaji hawa wazuri.” Alisema Ferguson.
Kwa Ronaldo mechi hiyo ilikuwa fursa ya kubeba kombe kwa mwaka wa pili mfululizo, kwa Messi ingekuwa kama ni mara ya kwanza licha ya kuwa kwenye timu iliyobeba taji hilo mwaka 2006 mjini Paris, Ufaransa lakini aliikosa mechi ya fainali baada ya kuwa majeruhi.
Kwa vyombo vya habari halikuwa suala la taji lililokuwa mbele ya timu hizo, pia walianza kutoa mwelekeo wa nani angetwaa tuzo ya mwanasoka bora wa Ulaya.
“Yoyote ambaye atatwaa taji hili atakuwa na nafasi nzuri,’’ alikiri Ronaldo lakini aliongeza, “hata hivyo hilo si jambo la muhimu, ninachokitaka kwa sasa ni kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya tu.”
Pia hakuna ambaye aliukwepa ukweli kwamba hiyo ilikuwa fursa nzuri kwa Messi kuwa mbele ya mpinzani wake mkuu ingawa mwenyewe hakuliona katika mtazamo huo, “Muhimu ni tuzo iliyo mbele ya timu, ukweli ni kwamba mshindi wa hapa Roma ndiye atakayekuwa timu bora ya Ulaya.
Mechi hiyo ilianza saa 2:46 kwa saa za Ulaya na Man United ilianza kwa kuwapa presha mapema wapinzani wao kwa kujaza washambuliaji nusu ya uwanja katika eneo la Barcelona wakati huo Barcelona wakihaha.
Ronaldo alikuwa tishio, alikuwa kichocheo cha kasi ya Man United uwanjani, lakini kwa upande wa pili, Messi hakuwa katika ubora wake jambo ambalo hata baba yake, Jorge naye aliliona.
Jorge alinukuliwa akisema, “nilimuona Leo, (Messi) hakuwa mchezoni kwa kipindi kirefu kidogo na ni pale tu tulipopata bao ndipo nilianza kumuona akiwa mchezoni.
Ukweli ni kwamba Messi alikuwa na mchango mdogo sana kwa timu yake, ni hadi pale Eto’o alipoipatia Barcelona bao la kwanza katika dakika ya kumi ndipo Messi alipoanza kufanya makeke yake.
Itaendelea Jumanne ijayo…