Medo, Lusajo wang'ara tuzo za Ligi Kuu Bara

MSHAMBULIAJI wa Namungo FC, Reliants Lusajo amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Desemba mwaka jana huku Kocha Mkuu wa Coastal Union Melis Medo akiwa Kocha bora.
Katika kikao chake cha kamati ya Tuzo za TFF kilichokutana Januari 4, mwaka huu kilimchagua Lusajo baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwa mwezi huo akifunga mabao matatu kwa timu yake na kuchangia Namungo kutoka nafasi ya 13 hadi ya nane, ikishinda michezo miwili, sare moja na kupoteza mmoja.
Kufuatia nyota huyo kushinda tuzo hiyo kunamfanya kuwa ni mchezaji wa nne msimu huu akitanguliwa na Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons (Novemba), Feisal Salum wa Yanga (Oktoba), na Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania kwa mwezi Septemba.
Lusajo ameshinda tuzo hiyo akiwashinda Saido Ntibazonkiza wa Yanga na Haji Ugando wa Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' huku kwa upande wa Medo amewashinda Pablo Franco (Simba) na Nasreddine Nabi wa Yanga alioingia nao fainali baada ya kuisaidia Coastal kushinda michezo mitatu na kupoteza mmoja ikitoka nafasi ya tisa mpaka ya nne.
Makocha wengine walioshinda tuzo hiyo ni Malale Hamsini wa Polisi Tanzania (Septemba), Nasreddine Nabi wa Yanga (Oktoba) na Salum Mayanga wa Tanzania Prisons (Novemba).
Katika hatua nyingine kamati ya tuzo imemchagua Meneja wa uwanja wa Azam Complex Chamazi Sikitu Kilakala kuwa meneja bora kwa mwezi huo, ikiwa ni kwa mara ya pili mfululizo kushinda.
Ushindi kwa Meneja huyo umefuatia kufanya kwake vizuri katika Menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.
Lengo la tuzo hiyo ni kuhamasisha mameneja wa viwanja kutilia mkazo masuala ya menejimenti ya matukio, kutuza na kusimamia miundombinu ya viwanja na taratibu nyingine zinazohusu mpira wa miguu viwanjani mwao.