Mechi ya Simba, Polisi yapigwa kalenda

Wednesday October 13 2021
mechi simba pic
By Ramadhan Elias

MCHEZO namba 24 wa Ligi Kuu Bara (TPL) kati ya Simba na Polisi Tanzania uliopangwa kuchezwa Oktoba 20, 2020 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa umeahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine.

Mechi hiyo ni ile ya mzunguko wa tatu wa TPL kwa msimu huu baada ya mechi mbili za mwanzo kwa kila timu huku Polisi ikiongoza Ligi baada ya kushinda zote na kujikusanyia alama sita kileleni na Simba ikiwa nafasi ya sita na alama nne baada ya kutoa sare moja na kushinda moja.

Taarifa kutoka Bodi ya Ligi iliyotolewa leo jioni imeeleza kuwa mechi hiyo haitachezwa Oktoba 20, na baadala yake itapigwa Oktoba 27 kwenye Uwanja ule ule wa Mkapa ambao Simba ndio watakuwa wenyeji.

Sababu za kuahirishwa kwa mechi hiyo zimeelezwa kuwa ni kutokana na Simba kukabiliwa na changamoto ya kupata usafiri wa haraka wa kurejea nchini kutoka Botswana ambako watacheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy, Oktoba 17, 2020.

Simba bado ipo nchini na Wikiendi hii itasafiri kuelekea Botswana kuwavaa Galaxy ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Wekundu wa Msimbazi hao katika michuano ya kimataifa msimu huu.

Advertisement