Mechi tatu za heshima KenGold

Muktasari:
- KenGold inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 16 ikiwa tayari imeshuka daraja baada ya kucheza mechi 27 ikishinda tatu, sare saba na vipigo 17, ndiyo timu inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 50 huku yenyewe ikifunga 22.
LICHA ya KenGold kushuka daraja, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Omary Kapilima amesema anataka kuacha maumivu ligi kuu kwa kuhakikisha anashinda michezo yote mitatu iliyosalia.
KenGold inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 16 ikiwa tayari imeshuka daraja baada ya kucheza mechi 27 ikishinda tatu, sare saba na vipigo 17, ndiyo timu inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 50 huku yenyewe ikifunga 22.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kapilima alisema kushuka kwao daraja haina maana wamemaliza msimu bali wana dakika 270 za kuipambania timu hiyo ishuke kwa heshima ikiacha vilio kwa timu ambazo zina uhakika wa kucheza msimu ujao.
"Tuna michezo muhimu mitatu na tunahitaji kuweka rekodi kwa kuonesha tumeshuka kwa kukosa mipango thabiti na sio kwamba hatuna uwezo, bado tunahitaji matokeo mazuri kwenye mechi tatu zilizobaki," alisema na kuongeza.
"Tunawaacha wana Mbeya vizuri na kurudi kujipanga upya, tutakuwa nyumbani mechi mbili na tutamaliza ugenini, mipango mikakati kwa ajili ya kujiweka sawa inaendelea na vijana wanatambua umuhimu wa mechi hizo."
Kapilima alisema KenGold imeshuka lakini kuna wachezaji bado matamanio yao ni kucheza ligi, hivyo anaamini watatumia mechi hizo tatu kujiweka sokoni kwa kuipambania timu kucheza kwa ubora na kuipa matokeo.
"Unajua mpira ni mchezo wa wazi, kila mmoja ameona namna tumeipambania hii timu, tumeangushwa na mambo machache lakini wachezaji wenye uwezo tuliwapata na wapo tayari kwa kuacha maswali kwenye mechi zilizobaki."
Timu hiyo itakuwa nyumbani Mei 13 mwaka huu ikiikaribisha Pamba Jiji iliyotoka kupoteza dhidi ya Simba kwa kukubali kichapo cha mabao 5-1 kwenye Uwanja wa KMC Jijini Dar es Salaam.
Baada ya hapo, Juni 18 KenGold itaikaribisha Simba, kisha itamaliza ugenini Juni 22 dhidi ya Namungo.