Mcolombia ampa mzuka kocha Azam FC

KURUDI uwanjani kwa mshambuliaji Franklin Navarro (24) kumempa mzuka Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo aliyekiri kumeongeza nguvu eneo hilo ambalo halikuwa na mtu baada ya kuondoka kwa Prince Dube.

Azam iliitambia Yanga kwa mabao 2-1 katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara kabla haijasimama bila ya kuwa na mshambuliaji halisi kutokana na Navarro kuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha tangu Februari, huku Dube akiwa na mgomo baridi akishinikiza kuondoka na Alassane Diao akifanyiwa upasuaji pia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dabo amesema kuna raha kikosini kutumia mfumo wa mshambuliaji japo aliweza kuwatumia wachezaji wengine na wakapata matokeo mazuri, huku akikiri kurudi kwa Navarro kutaongeza nguvu.

"Tumecheza mechi nyingi huku nyuma bila washambuliaji na tukapata matokeo lakini hilo haliondoi umuhimu wa mshambuliaji kikosini, kurudi kwake kutaongeza idadi ya mabao, hata asipofunga atahusika kuchangia timu kupata matokeo," amesema Dabo na kuongeza;

"Kurudi kwake ni chachu ya timu kuendeleza ushindani wa upachikaji mabao, ukiangalia timu zilizofunga mabao mengi sisi ni miongoni mwao, hivyo tutaendeleza hilo, lengo ni kuona mabao ndiyo yataamua kitu mwisho wa msimu bila kutegemea pointi."

Dabo akizungumzia maandalizi kwa jumla amesema wanaendelea kujifua tayari kwa ajili ya mwendelezo wa mechi za ligi huku akiweka wazi watakuwa ugenini kuikabili Namungo FC.

"Timu inaendelea na mazoezi tayari kwa ajili ya mechi za ligi ambazo zinarejea kuanzia wiki ijayo na sisi tutakuwa ugenini dhidi ya Namungo mchezo ambao ni muhimu kwetu kuendelea kujihakikishia nafasi ya ubingwa," amesema.

Azam ipo nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 20 ikishinda michezo 14, sare tano na kupoteza mechi mbili ikifanikiwa kukusanya pointi 47 nyuma ya vinara Yanga waliokusanya pointi 52 kupitia mechi 20 na Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45 kupitia michezo 19 tu.

Simba na Yanga kwa sasa zipo bize na mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo leo saa 3:00 usiku Wekundu watavaana na Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kesho Vijana wa Jangwani kuingia mzigoni kukabiliana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.