Gamondi avujisha majibu mtihani wa Mamelodi

Muktasari:

  • Kwa nini Gamondi? Licha ya kwamba Yanga ilitolewa na Mamelodi katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoka suluhu nyumbani na ugenini, kocha huyo alionyesha uwezo mkubwa wa kimbinu namna ya kukabiliana na mabingwa hao wa African Football League.

Yote hayo ameyataka Miguel Gamondi. Huko Afrika Kusini anatafutwa nani mchawi kufuatia mimba ya soka nchini humo, Mamelodi Sundowns kuondolewa katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis.

Kwa nini Gamondi? Licha ya kwamba Yanga ilitolewa na Mamelodi katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoka suluhu nyumbani na ugenini, kocha huyo alionyesha uwezo mkubwa wa kimbinu namna ya kukabiliana na mabingwa hao wa African Football League.

Gamondi aliisuka Yanga iliyokuwa na uwezo mzuri wa kuziba mianya ya Mamelodi Sundowns kuwadhuru, huku wakitumia kasi ya wachezaji wao kuutafuta mpira kuanzia katika eneo lao kitu ambacho kimeonekama pia kufanywa na Esperance ya Tunisia.

Hata kocha wa Mamelodi, Rhulani Mokwena, alikiri hilo na bahati mbaya kwao ni kwamba hawakuwa na mpango mbadala hata katika mchezo wa nusu fainali, jambo ambalo lilimfanya Miguel Cardos na vijana wake wa Esperance kujua wapi pa kuanzia.

Esperance ambayo ilikuwa bora kimbinu ilizima jana usiku, Ijumaa, matumaini ya Mamelodi kupindua matokeo ya bao 1-0 ambayo walifungwa ugenini ili kutinga fainali ya tatu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakiwa kwenye uwanja  wa nyumbani, Loftus Versfeld, jahazi la Mamelodi lilizamishwa dakika ya 57 na kijana mwenye miaka 20 Raed Bouchniba na safari ikawa imeishia hapo.

Kutolewa kwa Mamelodi katika hatua hiyo na Esperance imekuwa sherehe kwa baadhi ya mashabiki wa soka Tanzania kufuatia tukio la Yanga kunyimwa bao la Stephane Aziz KI katika mchezo wa marudiano uliopigwa Afrika Kusini, ambalo pengine lingewafanya Wananchi kutinga nusu.

Mara ya baada ya mchezo kati ya Mamelodi dhidi ya Esperance kumalizika Watanzania walikimbia katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za timu hiyo na kuanza kuwashambulia.

Matokeo ya mchezo wa nusu fainali ya pili yalishuhudia mabingwa mtetezi, Al Ahly ambao waliitoa Simba katika hatua ya robo fainali wakitinga fainali wakiwa nyumbani kufuatia mchezo wa kwanza uliopigwa Lubumbashi, DR Congo kutoka suluhu.

Ahly imetinga hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, hivyo fainali ya msimu huu katika Ligi ya Mabingwa itakuwa kati ya Mafarao hao dhidi ya Esperance ambao pia nao ni wababe katika michuano hiyo.

Esperance imewahi kutwaa ubingwa 2018 mbele ya Ahly katika mchezo wa fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3. Fainali ya kwanza msimu huu itachezwa Mei 18, huku marudiano ikiwa Mei 25.