Baraza afichua kilichoiua KMC

Muktasari:

  • Dodoma ilipata ushindi huo kwa bao la Paul Peter dakika ya tisa tu ya mchezo huo uliopigwa juzi Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ikiwa ni kichapo cha pili kwa KMC kukipata baada ya mechi ya kwanza kuchapwa mabao 2-1, Novemba 3, mwaka jana.

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji Mkenya, Francis Baraza amesema sababu kubwa ya timu hiyo kushinda bao 1-0 dhidi ya KMC ni kutokana na kutumia mipira mirefu wakati wa kushambulia jambo ambalo lilikuwa ni changamoto zaidi kwa wapinzani wao.

Dodoma ilipata ushindi huo kwa bao la Paul Peter dakika ya tisa tu ya mchezo huo uliopigwa juzi Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ikiwa ni kichapo cha pili kwa KMC kukipata baada ya mechi ya kwanza kuchapwa mabao 2-1, Novemba 3, mwaka jana.

Akizungumza na Mwanaspoti Baraza amesema walitambua wapinzani wao ni wazuri wakati wakiwa na mpira, lakini wakipoteza si wepesi wa kukaba kwa haraka jambo walilolitumia na kuzaa matunda kwa kutumia mawinga wenye kasi.

"Kucheza na KMC sio kitu kidogo kwa sababu ina vijana wasumbufu na wanaoweza kuchezea mpira ila shida yao niliyoiona sio wazuri wanapokuwa hawana mpira mguuni, udhaifu ambao tuliutumia ndio maana tukaimaliza mechi mapema tu," amesema.

Rekodi zinaonyesha timu hizi zimekutana katika michezo minane ya Ligi Kuu Bara tangu msimu wa 2020/2021 ambapo Dodoma imekuwa mbabe zaidi kwani imeshinda sita, kati ya hiyo, huku KMC ikishinda miwili.

Matokeo hayo yameifanya Dodoma kutoka nafasi ya 10 hadi ya nane kwenye msimamo ikiwa na pointi 28 katika michezo 23 huku KMC iliyokuwa inacheza mechi ya 24 msimu huu imeendelea kusalia nafasi ya tano kwa kuwa na pointi 32.