Mbili zabaki vita ya ubingwa ZPL, Mwenge yapumulia mashine

Muktasari:
- Timu zilizoshuka daraja ni Tekeleza, InterZanzibar na New City huku ikisubiriwa moja kukamilisha ya nne zinazotakiwa kushuka.
WAKATI ukibaki mzunguko mmoja wa kuhitimisha msimu huu wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), timu mbili pekee zimesalia katika vita ya kuwania ubingwa, huku Mwenge ikiwa hatarini kushuka.
Kwa sasa Mlandege inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 59 sawa na KVZ inayoshika nafasi ya pili huku zikitofautishwa kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mlandege katika mechi 29 ilizocheza na kukusanya pointi 59, imefunga mabao 63 na kuruhusu 19 tofauti mabao 44 wakati KVZ ikifunga 34 na nyavu zake kutikiswa mara 12, tofauti mabao 22.
Mlandege ambayo ina asilimia kubwa ya kutwaa ubingwa huo endapo ikishinda mechi ya mwisho, jana Juni 3, 2025 imevuna alama tatu baada ya kuitembezea Kipanga kichapo cha mabao 3-0.
Laurent Rolenzo aliitangulizia Mlandege akifunga bao la kwanza dakika ya 30, Abdallah Iddi 'Pina' aliweka bao la pili dakika 51 na na Mussa Hassan akahitimisha ushindi huo dakika ya 65.
Mshambuliaji wa Mlandege, Pina ameendelea kujitengenezea nafasi ya kutwaa Tuzo ya Ufungaji Bora baada ya kufikisha mabao 19.
KVZ inayotunishiana misuli na Mlandege, nayo imeichapa Muembe Makumbi mabao 2-1 na kuiondosha rasmi kwenye vita ya kuwania ubingwa.
Mabao yote ya KVZ yaliyozima matumaini ya Muembe Makumbi kuwania ubingwa yamefungwa na Michael Joseph dakika ya 56 na 66, huku Muembe Makumbi ikipata bao la kufutia machozi dakika ya 78 lililowekwa wavuni na Robert Pius.
Kesho Alhamisi Juni 5, 2025, Mlandege itamaliza dhidi ya New City iliyoshuka daraja wakati Ijumaa Juni 6, 2025 KVZ ikivaana na Kipanga ambayo haina inachotafuta, mechi hizo zitaamua bingwa wa msimu wa 2024-25.
Ligi hiyo itaendelea leo Jumatano Juni 4, 2025 ambapo Mwege yenye pointi 35 itacheza dhidi ya InterZanzibar ambayo tayari imeshashuka daraja.
Mwenge inahitaji ushindi wa lazima katika mchezo huo ili kufikisha pointi 38, kisha iombe Junguni United ipoteze ili kuepuka kushuka daraja.
Kwa sasa Junguni ina pointi 37 ikishika nafasi ya 12, ambapo mechi ya mwisho leo Jumatano Juni 4, 2025 itakabiliana na KMKM.