Fainali Shirikisho yarudishwa Zanzibar

Muktasari:
- Ikumbukwe kuwa, Fainali iliyopita kati ya Azam dhidi ya Yanga ilichezwa uwanja huo na Yanga kutetea ubingwa wake kwa mikwaju ya penalti.
ILE Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kati ya Yanga dhidi ya Singida Black Stars, wakati wowote inaweza kurejea Zanzibar,huku tarehe ikiwa bado haijajulikana.
Ikumbukwe kuwa, Fainali iliyopita kati ya Azam dhidi ya Yanga ilichezwa uwanja huo na Yanga kutetea ubingwa wake kwa mikwaju ya penalti.
Taarifa kutoka ndani ya TFF ni kwamba mchakato huo ulikumbana na machaguo mawili pekee ya wapi mchezo huo utapigwa ambapo viwanja vilivyo pendekezwa vilikuwa CCM Kirumba Jijini Mwanza na Amaan Zanzibar.
Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa Uwanja wa Kirumba haukuwaridhisha maafisa waliokwenda kuukagua, hali iliyosababisha chaguo libaki Uwanja wa Amaan pekee.
Taarifa za ndani zinasema kuwa, mabosi wa CRDB ambao ndio wadhamini wa mashindano hayo nao walikuwa na mapendekezo ya fainali hiyo kurudishwa Zanzibar.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Mohammed Kambangwa alizungumza na Mwanaspoti na kuliambia kuwa;"Hizo taarifa tunazisikia hazijawa rasmi sana zinazunguka maeneo mbalimbali, lakini zitakapokuwa rasmi, tutawajulisha mara moja."
Licha ya taarifa za uhakika kudai kwamba mchezo huo utapigwa Uwanja huo wa Amaan, lakini bado tarehe rasmi ilikuwa haijawekwa wazi.
Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi alizungumzia na Mwanaspoti na kuliambia kuwa;"Wakati wowote tutatangaza rasmi wapi mchezo huo utachezwa," alisema Madadi ambaye idara yake ndiyo inayoratibu mashindano hayo.
Yanga inakutana na Singida Black Stars baada ya kuwachapa JKT Tanzania, katika hatua ya nusu fainali mabao 2-0, huku Singida ikiwatoa Simba kwa kipigo cha mabao 3-1.