Mbeya City yarejea Ligi Kuu kwa kishindo

Muktasari:
- Mbeya City imerejea Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa misimu miwili tangu iliposhuka msimu wa 2022-2023 ilipomaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo, kisha kupoteza mechi za play off dhidi ya KMC na Mashujaa.
USHINDI wa mabao 5-0 ilioupata Mbeya City dhidi ya Cosmopolitan, umeifanya timu hiyo kutoka jijini Mbeya kurejea Ligi Kuu Bara msimu ujao 2025-2026 baada ya kufikisha pointi 65 ambazo haziwezi kufikiwa na timu inayoshika nafasi ya kuanzia ya tatu kushuka chini.
Mbeya City imerejea Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa misimu miwili tangu iliposhuka msimu wa 2022-2023 ilipomaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo, kisha kupoteza mechi za play off dhidi ya KMC na Mashujaa.
Katika mchezo uliochezwa leo Mei Mosi 2025 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wafungaji wa mabao yaliyoirudisha Mbeya City ligi kuu ni Riphat Khamis aliyepachika mawili, Eliud Ambokile, Faraji Kilaza Mazoea na David Mwasa kila mmoja wakifunga mojamoja.
Ikiwa kila timu imebakiza mechi moja kumaliza msimu wa 2024-2025 kwenye Ligi ya Championship, pointi ilizonazo Mbeya City haziwezi kufikiwa na Stand United inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 60 kwenye mechi 29 ilizocheza.
Stand United ilikuwa na nafasi ya kuendelea kuisubirisha Mbeya City hadi mchezo wa mwisho, lakini sare ya bao 1-1 waliyoipata dhidi ya Polisi Tanzania imeifanya kuiachia nafasi Mbeya City kupanda sambamba na Mtibwa Sugar ambayo ilikuwa ya kwanza ikiwa ndiyo kinara wa ligi hiyo na pointi 68.
Mbeya City mara ya kwanza kushiriki Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu wa 2013-2014 ambapo ilicheza ligi hiyo kwa misimu kumi mfululizo kisha ikashuka 2022-2023.
Wakati Mtibwa Sugar na Mbeya City zikipanda daraja, Stand United na Geita Gold, zitacheza mechi za play off kupambania nafasi moja ya kucheza Ligi Kuu Bara kutokana na pointi zao kuwafanya kuwa na uhakika wa kumaliza nafasi ya tatu na nne.
Kwa upande mwingine, Biashara United imeshuka na msimu ujao itashiriki First League kutokana na kuwa na pointi 15 ikibakiza mchezo mmoja ambao hata ikishinda, haiwezi kutoka nafasi mbili za chini ambazo timu hushuka daraja moja kwa moja.
MATOKEO YA MECHI ZA CHAMPIONSHIP LEO MEI 1, 2025
Biashara United 1-1 Geita Gold
Polisi Tanzania 1-1 Stand United
African Sports 2-0 Kiluvya FC
Transit Camp 2-2 Mtibwa Sugar
Mbeya City 5-0 Cosmopolitan
Songea United 2-1 Green Warriors
Mbeya Kwanza 0-0 TMA FC
Mbuni FC 1-1 Bigman FC