Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeya City yaanza usajili Ligi Kuu Bara, Malale naye ndani

CITY Pict

Muktasari:

  • Pia imesema baada ya kufanikiwa kutimiza malengo ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao, itaandaa sherehe Mei 31 kupongezana kutimiza malengo.

Timu ya Mbeya City imesema wakati ikiendelea na usajili, lakini upande wa benchi la ufundi imeshamalizana na Kocha Mkuu, huku ikikiri wapo wachezaji watakaoachwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo matakwa yao.

Pia imesema baada ya kufanikiwa kutimiza malengo ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao, itaandaa sherehe Mei 31 kupongezana kutimiza malengo.

Akizungumza leo Jumapili Mei 25, Mtendaji Mkuu wa Mbeya, Ally Nnunduma amesema sehemu ya benchi la ufundi litakuwa na maboresho lakini si kwa kocha Mkuu kwa kuwa walishamalizana na Malale Hamsini aliyechukua mikoba ya mtangulizi wake, Salum Mayanga.

Nnunduma amesema kwa sasa tayari wanaendelea na usajili na tayari baadhi ya mastaa waliofanya vizuri wameshaongezewa mkataba na wengine wakiendelea na mazungumzo nao akieleza kuwa mkakati wao ni kuwa timu yenye ushindani na kuendeleza heshima Uwanja wa Sokoine.

"Nilisema mapema kwamba, kocha Mkuu anayekuja tuwe naye Ligi Kuu, hivyo kama yatakuwapo maboresho tutawaambia ila kocha Mkuu tunaye Malale na wachezaji waliong'ara tutabaki nao, labda wale watakaogoma kwa matashi yao," amesema Nnunduma na kuongeza; 

"Tayari baadhi tumewapa mkataba mpya na wengine mazungumzo yanaendelea, tutasajili timu bora ili kuweka ushindani, tunataka Sokoine iwe ya heshima kwa timu yoyote inayokuja inaacha pointi tatu."

Kigogo huyo ameongeza  baada ya kufanikiwa kurejea Ligi Kuu, wadau wa timu hiyo wameandaa sherehe maalumu itakayofanyika Mei 31 kupongeza wachezaji kutimiza malengo hayo.

Mchumi huyo wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ameeleza  wanatarajia kuanza maandalizi mapema ikiwamo kambi binafsi ya timu na uwanja wa mazoezi ili kutengeneza kikosi chenye ubora wa kushindana.

"Mbali na pati hiyo ya Mei 31, mashabiki pia wameandaa burudani nyingine Juni 14 kule Matema Beach, uongozi tumejipanga timu kutokaribia kucheza play off badala yake kuwa nafasi nzuri," amesema Mtendaji huyo na kuongeza;

"Ipo pia akademi tumeandaa na tutaizindua muda wowote sambamba na uwanja wa mazoezi, tutasajili wachezaji wenye ubora bila kujali sehemu atokayo na uwezo tunao wa kumleta mchezaji yeyote kutoka nchi yoyote."

Bosi huyo, hakusita kuwashukuru wadau na mashabiki waliofanikisha kusaidia mafanikio hayo, huku akieleza kuwa uongozi umejitajidi kulipa madeni yote hadi kumaliza msimu wa Ligi ya Championship.