Mbappe anukia Juventus

TURIN, ITALIA. UKARIBU kati ya Cristiano Ronaldo na Kylian Mbappe kuna kitu kinaendelea mjue, wakati Mbappe anamtaja Ronaldo kama mchezaji anayemkubali na kujifananisha naye, ripoti zinadai kwamba Juventus inataka kulipa Euro 400 milioni ili kuvunja mkataba wa staa huyo wa PSG katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Kupitia tovuti ya Tuttosport, inaelezwa Juve ina itamani sana saini ya Mbappe na inaamini atakuwa bora zaidi na msaada kwa timu ikiwa atajiunga nao na kucheza sambamba na Ronaldo ambaye ni mchezaji anayemkubali.

Kwa sasa Juve inapambana kuhakikisha inaandaa kiasi cha pesa ambacho kitatumika mwakani kuvunja mkataba wa fundi huyo mwenye umri wa miaka 21.

lakini kusajiliwa kwa Mbappe kunaweza kutoa nafasi ya PSG kufanikisha mchakato wa kuipata saini ya Ronaldo ambayo pia imekuwa ikitamani kwa muda mrefu hivyo kuna uwezekano Juve isitoe Euro 400 milioni yote kwa ujumla kama ambavyo PSG ilitangaza kwa klabu zinazohitaji saini yake kwa sababu zinaweza kufanya mabadilishano ya wachezaji na kikatumika kiasi kidogo cha pesa.

Msimu ujao Ronaldo atakuwa anafikisha umri wa miaka 36 na mkataba wake utakuwa umebakisha mwaka mmoja lakini bado anaendelea kuonesha kiwango kikubwa huku Mbappe yeye atakuwa anafikisha umri wa miaka 22 na mkataba wake utakuwa umebakisha mwaka mmoja.

Mbappe amekuwa kwenye kiwango kikubwa kinachozifanya klabu nyingi kutamani saini yake na msimu huu amefunga mabao mawili na kutoa asisti nne katika michezo mitatu ambayo ametumia dakika 259.

Inaaminika kuwa Juve inaweza kumtumia Ronaldo ili amshawishi Mbappe ajiunge nao kwa sababu mchezaji huyo anamkubali sana.

Mbappe ni moja ya wachezaji waliofanikiwa kupata mafanikio makubwa kwenye soka hasa baada ya kufanikiwa kuiwezesha taifa lake la Ufaransa kubeba Kombe la Dunia mwaka 2018 baada ya kuichapa Croatia mabao 4-2 kwenye fainali iliyofanyika Russia na baada ya hapo amekua akiwindwa na klabu kubwa kwa muda mrefu.